
JERUSALEM – Waziri Mkuu wa mpito wa Israel, Benjamin Netanyahu, ametoa wito wa kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa kwa kushirikiana na mpinzani wake wa kisiasa, Gadi Eisenkot, lakini pendekezo hilo limepingwa na Eisenkot aliyelitaja kuwa mbinu ya kisiasa yenye lengo la kuchelewesha mchakato wa kuunda serikali mpya.
Mvutano huo umeibuka wakati Eisenkot akiendelea na mazungumzo ya kuunda serikali mpya baada ya kuteuliwa Jumapili iliyopita kupewa jukumu la kuunda serikali ndani ya siku 28, huku akipewa uwezekano wa kuongezewa siku nyingine 14.
Akizungumza kupitia video, Netanyahu amesema mazungumzo aliyofanya na Eisenkot siku ya Alhamisi yamempa imani zaidi kwamba Israel inahitaji serikali ya umoja wa kitaifa ili kuimarisha usalama wa nchi hiyo.
Amedai serikali hiyo inaweza kukabiliana na changamoto za kiusalama, hususan tishio kutoka Iran, ambalo amesema linaweza kuhatarisha usalama wa Israel.

Netanyahu amependekeza serikali hiyo ihusishe vyama vinavyotambua Israel kama taifa la watu wa Kiyahudi, akionya kuwa mpango wa Eisenkot wa kuunda serikali ya wachache unaweza kuwa dhaifu na kuhatarisha usalama wa nchi.
Kwa mujibu wa mgawanyo wa wabunge katika Bunge la Israel (Knesset), muungano unaoungwa mkono na Eisenkot una wabunge 48, huku upande wa Netanyahu ukiwa na wabunge 46. Wabunge wengine 26 kutoka vyama vya Waarabu na vya Kiorthodoksi wanaweza kujizuia kupiga kura, jambo linaloweza kuruhusu serikali ya Eisenkot kuundwa bila kupata uungwaji mkono wa zaidi ya nusu ya wabunge wote 120.
Hata hivyo, Eisenkot amejibu kwa kumshutumu Netanyahu kwa kutumia mbinu za kisiasa, akisema anafahamu kuwa ameshindwa uchaguzi na sasa anajaribu kutumia wito wa serikali ya umoja kuvuruga mchakato unaoendelea wa kuunda serikali mpya.
Amesema Netanyahu anazungumzia mazungumzo ya kisiasa wakati mazungumzo hayo tayari yanaendelea, huku akituhumu kuwa kauli zake kuhusu umoja haziendani na mwenendo wake wa kisiasa unaochochea mgawanyiko.
EISENKOT ATAKA KUACHANA NA WAPIGANIA MIKAKATI YA MRENGO MKALI
Katika hatua nyingine, Eisenkot amesisitiza kuwa serikali atakayoiongoza lazima ijitenge na wanasiasa wenye misimamo mikali, hususan wafuasi wa Waziri wa Usalama wa Taifa, Itamar Ben Gvir.
Amesema yuko tayari kushirikiana na baadhi ya wanachama wa chama cha Likud cha Netanyahu pamoja na chama cha Religious Zionism kinachohusishwa na Waziri wa Fedha anayemaliza muda wake, Bezalel Smotrich, iwapo wataonyesha nia ya dhati ya kushiriki katika serikali ya umoja.
Hata hivyo, uwezekano wa Eisenkot kuunda serikali moja kwa moja na Netanyahu bado unaonekana kuwa mgumu, hasa baada ya kumkosoa Netanyahu kwa kile alichokiita kampeni ya kibaguzi dhidi ya vyama vya Waarabu nchini Israel.
Eisenkot pia ameitaka kambi ya Likud na washirika wake kuunga mkono uteuzi wa Matan Kahana kuwa Spika wa Bunge la Israel, badala ya kuendelea kumuunga mkono Amir Ohana, ambaye ni mshirika wa karibu wa Netanyahu na ndiye anayeshikilia nafasi hiyo kwa sasa.
Mvutano huo wa kisiasa unaendelea kuonyesha changamoto zinazomkabili Eisenkot katika jitihada zake za kuunda serikali mpya, huku suala la ushirikiano wa vyama vya Kiyahudi na vya Waarabu likiwa miongoni mwa masuala yanayogawa wanasiasa wa Israel.