
WASHINGTON, MAREKANI – Rais wa Marekani, Donald Trump, ameunga mkono juhudi za kumrejesha Jensen Huang katika nafasi ya Mtendaji Mkuu (CEO) wa kampuni ya teknolojia ya Nvidia, siku chache baada ya kujiuzulu kutokana na sakata la mahusiano yake ya kimapenzi na tuhuma zinazohusishwa na usalama wa taifa.
Trump amesema hatakuwa na pingamizi iwapo bodi ya kampuni hiyo itaamua kumrejesha Huang katika nafasi hiyo, akieleza kuwa aliyekuwa kiongozi huyo amejifunza somo kutokana na yaliyotokea.
Kauli hiyo imekuja wakati kampeni inayojulikana kama Stand with Jensen ikiendelea kupata uungwaji mkono kutoka kwa wafanyakazi wa zamani na wa sasa wa Nvidia, wawekezaji pamoja na baadhi ya watu mashuhuri katika sekta ya teknolojia ya Silicon Valley.

Miongoni mwa waliounga mkono kampeni hiyo ni bilionea Elon Musk, mmiliki wa SpaceX, na Tim Sweeney, Mtendaji Mkuu wa kampuni ya Epic Games.
Musk aliandika kwenye mtandao wa X kuwa anasaini ombi hilo, huku Sweeney akitoa ujumbe wa kumtaka Huang aokolewe na kurejeshwa katika nafasi yake.
Kampeni hiyo inaitaka bodi ya Nvidia kumrejesha Huang wakati uchunguzi huru ukiendelea au hadi pale ushahidi wa kutosha utakapothibitisha kuwa kuondoka kwake ni kwa manufaa ya kampuni.

Hata hivyo, taarifa kutoka kwa mtu anayefahamu msimamo wa bodi ya Nvidia, aliyenukuliwa na Associated Press kwa sharti la kutotajwa jina, zinaeleza kuwa bodi hiyo haifikirii kwa sasa kumrejesha Huang.
Huang alijiuzulu wiki iliyopita baada ya kufichuka kwa taarifa kuhusu madai ya kuwa na mahusiano ya kimapenzi nje ya ndoa na wanawake wawili, mmoja akiwa mfanyabiashara raia wa China anayeshukiwa kuwa na uhusiano na vyombo vya kijasusi vya Beijing, na mwingine akiwa mtendaji mkuu wa kampuni aliyekuwa chini ya usimamizi wake.
Taarifa hizo zimeibua mjadala mkubwa kuhusu maadili ya uongozi, usimamizi wa kampuni na masuala ya usalama wa taifa la Marekani.
Trump, hata hivyo, amepunguza uzito wa tuhuma hizo, akisema bado hakuna aliyethibitisha kuwa mwanamke huyo alikuwa jasusi.
Kwa upande mwingine, Waziri wa Fedha wa Marekani, Scott Bessent, amekuwa na msimamo tofauti na Trump, akitaka kufanyika kwa mabadiliko makubwa katika uongozi wa Nvidia na kupendekeza kiongozi mpya atoke nje ya kampuni hiyo.
Wakati sakata hilo likiendelea, Afisa Mkuu wa Fedha wa Nvidia, Colette Kress, amechukua nafasi ya Mtendaji Mkuu wa muda wakati bodi ikiendelea na mchakato wa kutafuta mrithi wa Huang.
Kutokana na sintofahamu kuhusu mustakabali wa kampuni hiyo, hisa za Nvidia zilishuka kwa asilimia 4.1 mwishoni mwa biashara ya Jumatatu, hali iliyochangia kushuka kwa fahirisi ya S&P 500 kwa karibu asilimia mbili.
Huang alikuwa miongoni mwa watu muhimu walioijenga Nvidia kuwa kampuni kubwa ya teknolojia ya kimataifa baada ya kuianzisha zaidi ya miongo mitatu iliyopita. Kampuni hiyo ina nafasi muhimu katika ukuaji wa teknolojia ya akili unde (AI), huku bidhaa zake za chip zikitumika katika vituo vya kuhifadhi na kuchakata data pamoja na mifumo ya kompyuta inayotumia teknolojia hiyo.
Akizungumzia sakata hilo, Mtendaji Mkuu wa OpenAI, Sam Altman, alisema Huang amekuwa mtu anayemheshimu kwa muda mrefu, lakini alieleza kuwa hana taarifa za kutosha kuamua iwapo anapaswa kurejeshwa katika nafasi yake.
Aliongeza kuwa watu wanaoheshimiwa pia wanaweza kuwa na mapungufu, huku akimpongeza Huang kwa kampuni aliyoijenga.
Kwa sasa, hatma ya Huang katika Nvidia bado haijafahamika, huku kampeni ya kumrejesha ikiendelea kukutana na maswali kuhusu maadili ya kampuni, usalama wa taifa na uwajibikaji wa viongozi wakuu wa biashara.