
ZIMBABWE – Uchunguzi wa ajali ya helikopta iliyosababisha kifo cha mfanyabiashara maarufu wa Zimbabwe, Wicknell Chivayo, mke wake na watu wengine watatu umeingia katika changamoto baada ya kifaa cha kurekodi mawasiliano ya marubani, kinachojulikana kama Black Box, kutopatikana katika mabaki ya ndege hiyo.
Ripoti ya awali iliyotolewa na Idara ya Uchunguzi wa Ajali na Matukio ya Anga chini ya Wizara ya Uchukuzi na Maendeleo ya Miundombinu nchini Zimbabwe imeeleza kuwa helikopta aina ya Bell 430, yenye usajili Z-PED, ilikuwa imefungwa kifaa cha kurekodi sauti za ndani ya chumba cha marubani (Cockpit Voice Recorder – CVR), lakini kifaa hicho hakikupatikana katika eneo la ajali na kinadhaniwa kuwa kiliharibiwa.

Kifaa hicho ni muhimu katika uchunguzi wa ajali za ndege kwa kuwa hurekodi mazungumzo ya marubani, mawasiliano yao na vituo vya udhibiti wa safari za anga, sauti za tahadhari pamoja na milio mingine ndani ya chumba cha marubani.
Kutopatikana kwake kunaweza kufanya iwe vigumu kwa wachunguzi kubaini kwa usahihi mawasiliano yaliyofanyika na hatua zilizochukuliwa na marubani wakati helikopta hiyo ilipokutana na hali mbaya ya hewa kabla ya kuanguka.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa ajali hiyo ilitokea Septemba 30 katika shamba la Kudenga, eneo la Mashonaland Mashariki, nchini Zimbabwe, huku uchunguzi wa awali ukibainisha kuwa ukungu, mawingu ya chini na uoni hafifu vilikuwa miongoni mwa mazingira yaliyokuwepo kabla ya ajali.
Wachunguzi pia wameeleza kuwa ajali hiyo haikuwa na uwezekano wa manusura kutokana na nguvu kubwa ya msukumo wakati helikopta ilipogonga ardhi pamoja na moto uliozuka baada ya ajali.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, helikopta hiyo ilivunjika vipande baada ya kugonga ardhi na moto uliteketeza sehemu kubwa ya mabaki yake. Watu wote waliokuwamo ndani walifariki dunia.
Taarifa zinaeleza kuwa helikopta mbili, moja aina ya Bell 407 yenye usajili Z-OSM na nyingine Bell 430 iliyokuwa imewabeba Chivayo na wenzake, ziliondoka katika Kijiji cha Gandami majira ya saa 8:20 mchana kwa safari binafsi kuelekea Marondera.
Ndege hizo zilikuwa zikiruka pamoja kwa kufuata taratibu za safari za anga zinazoendeshwa kwa mwonekano wa moja kwa moja.
Hata hivyo, takribani dakika 10 baada ya kuanza safari, mawingu mazito yalionekana yakikaribia kutoka upande wa mashariki, hali iliyosababisha helikopta ya Bell 407 kugeuka kuelekea magharibi ili kuepuka mawingu hayo.
Kwa mujibu wa ripoti, helikopta ya Bell 430 iliendelea kuelekea kaskazini-mashariki baada ya kutoa taarifa kuwa njia hiyo ilikuwa wazi.
Baadaye, mawasiliano ya mwisho kutoka kwa Bell 430 yalionyesha kuwa ilikuwa imeingia katika tabaka jingine la mawingu na ilikuwa bado haijatoka upande wa pili.
Mashuhuda katika shamba la Kudenga walisema walisikia sauti ya helikopta ikipita juu yao majira ya saa 8:50 mchana, lakini hawakuweza kuiona kutokana na mvua ndogo na ukungu mzito.
Walisema sauti hiyo iliendelea kwa takribani dakika 10 kabla ya kusikika kishindo kikubwa, kisha ukimya kutawala eneo hilo.
Polisi walipata taarifa za ajali hiyo majira ya saa 9:00 alasiri na kufika eneo la tukio dakika 15 baadaye, ambapo walithibitisha kuwa helikopta ilikuwa imeanguka na hakukuwa na manusura. Baadhi ya mabaki yake yalikuwa bado yanawaka moto.
Uchunguzi umebaini kuwa vipande vya helikopta vilisambaa katika eneo lenye urefu wa takribani mita 170 na upana wa mita 75, hali inayoonyesha ukubwa wa uharibifu uliotokea wakati wa kugonga ardhi.
Ripoti hiyo imesema hakuna ushahidi ulioonyesha kuwa helikopta ilivunjika ikiwa bado angani au kulikuwa na mlipuko kabla ya kugonga ardhi.
Aidha, hali mbaya ya hewa iliyokuwepo nchini Zimbabwe wakati huo imetajwa kuwa sehemu muhimu ya uchunguzi. Idara ya Hali ya Hewa ilikuwa imetoa tahadhari ya mvua kubwa, radi, upepo mkali na mvua za ghafla katika kipindi cha Septemba 29 hadi Oktoba Mosi.
Pamoja na changamoto ya kutopatikana kwa kifaa cha kurekodi mawasiliano ya marubani, wachunguzi wamefanikiwa kukusanya mabaki ya helikopta na kuyahifadhi katika eneo maalumu kwa uchunguzi zaidi.
Pia wamekusanya nyaraka za ndege, taarifa za matengenezo na kumbukumbu za usalama wa safari za anga. Mahojiano ya awali yamefanyika na wafanyakazi wa helikopta iliyokuwa ikiambatana na ndege iliyopata ajali, mashuhuda pamoja na watu waliofika kwanza eneo la tukio.
Ripoti hiyo imesema hadi sasa hakuna ushahidi ulioonyesha kuwa hali ya kiafya au kupoteza uwezo wa kufanya kazi kwa marubani kulichangia ajali hiyo.
Hata hivyo, wachunguzi wameonya kuwa ripoti hiyo ni ya awali na haijatoa hitimisho la mwisho kuhusu chanzo cha ajali.
Uchunguzi unaendelea kwa kuzingatia viwango vya kimataifa vya usalama wa usafiri wa anga, huku ripoti ya mwisho ikitarajiwa kutolewa baada ya kukamilika kwa uchambuzi wa kitaalamu na kubainishwa kwa mapendekezo ya kuzuia ajali zinazofanana na hiyo siku zijazo.