
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Camillus Wambura, amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu kupitia vituo vya polisi ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa kudhibiti vitendo vya uhalifu nchini.
IGP Wambura ametoa wito huo Novemba 17, 2026, akiwa katika Wilaya za Bagamoyo mkoani Pwani na Korogwe mkoani Tanga, wakati wa uwekaji wa mawe ya msingi ya ujenzi wa vituo vya polisi katika wilaya hizo.
Amesema ushirikiano kati ya wananchi na vyombo vya ulinzi na usalama ni muhimu katika kupambana na uhalifu, akisisitiza kuwa jamii ina jukumu la kutoa taarifa mapema pale inapobaini viashiria vya uhalifu au watu wanaojihusisha na vitendo hivyo.

Aidha, amewakumbusha askari polisi kote nchini kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na kuzingatia misingi ya haki ili kudhibiti uhalifu pamoja na kutatua changamoto zinazowakabili wananchi.
Ujenzi wa vituo hivyo ni sehemu ya jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita katika kuboresha miundombinu ya Jeshi la Polisi kwa kujenga vituo bora na vya kisasa katika maeneo mbalimbali nchini.
Hatua hiyo inalenga kuimarisha utendaji wa Jeshi la Polisi, kurahisisha upatikanaji wa huduma za kipolisi na kuongeza ufanisi katika kulinda usalama wa raia na mali zao.