
Meli ya MV Mwanza imepata ajali ndogo leo, Novemba 18, 2026, majira ya saa 4 asubuhi, wakati wa majaribio yaliyokuwa yakifanyika kabla ya kuanza rasmi kutoa huduma za usafiri katika Ziwa Victoria.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi wa Polisi (CP) Salum Hamduni amewahakikishia wananchi kuwa meli hiyo iko salama, akieleza kuwa uchunguzi wa awali uliofanywa na wataalamu umeonesha kuwa hakuna sababu ya wananchi kuwa na hofu kuhusu usalama wake.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu huyo wa Mkoa amesema tukio hilo limetokea wakati meli hiyo ikiwa katika hatua za majaribio, baada ya kukaa kwa muda mrefu bila kuanza safari za kawaida.

Ameeleza kuwa Serikali kupitia Shirika la Meli Tanzania (TASHICO) imekuwa ikiendelea na maandalizi ya kuhakikisha meli hiyo inaanza kutoa huduma kwa mujibu wa ratiba zilizopangwa.
Kufuatia tukio hilo, Mkuu wa Mkoa amesema tayari mawasiliano yamefanyika na Wizara ya Uchukuzi, ambayo imeelekeza kufanyika kwa uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo cha ajali hiyo na kiwango cha madhara yaliyotokea.
Ameongeza kuwa timu maalumu ya wataalamu itaundwa kwa kushirikisha Wizara ya Uchukuzi, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na mamlaka nyingine za Serikali ili kufanya tathmini ya kina kuhusu tukio hilo.

Aidha, amesisitiza kuwa Serikali itatoa taarifa rasmi kwa wananchi mara baada ya uchunguzi kukamilika na kubainika kwa chanzo halisi cha tukio hilo.
Katika hatua nyingine, amewataka wananchi kuendelea kuwa watulivu na kuepuka kusambaza taarifa ambazo hazijathibitishwa, akisisitiza kuwa taarifa sahihi kuhusu hali ya meli hiyo zitatolewa na mamlaka husika.
Tukio hilo limetokea wakati wananchi wakisubiri kuanza kwa huduma za MV Mwanza, meli inayotarajiwa kuwa sehemu muhimu ya usafiri na usafirishaji wa bidhaa katika Ziwa Victoria.