×

Elon Musk Ajutia Kutumia zaidi ya Trilioni 1 Kufadhili Wagombea wa Republican

Bilionea na mmiliki wa kampuni za Tesla na SpaceX, Elon Musk.

Bilionea na mmiliki wa kampuni za Tesla na SpaceX, Elon Musk, amekiri kujutia kiasi kikubwa cha fedha alichotumia kuunga mkono wagombea wa chama cha Republican katika uchaguzi wa katikati ya muhula nchini Marekani, baada ya wengi wa wagombea aliowafadhili kushindwa katika uchaguzi huo.

Musk amesema iwapo angepata nafasi ya kufanya upya maamuzi yake, angetumia fedha kidogo kuliko alizotumia katika kampeni hizo, ambazo zinakadiriwa kugharimu zaidi ya TSh trilioni 1.1.

Akizungumza Jumatano katika mkutano wa DealBook Summit ulioandaliwa na gazeti la The New York Times, kupitia mahojiano ya mtandaoni akiwa nchini China, Musk amesema anajutia matumizi hayo kutokana na matokeo kutolingana na kiasi kikubwa cha fedha alichowekeza.

“Ninajisikia mjinga kwa kutumia fedha nyingi kiasi hicho na kutopata matokeo makubwa. Au labda hali ingekuwa mbaya zaidi kama nisingetumia fedha hizo,” alisema Musk.

Bilionea huyo alikuwa mfadhili mkubwa zaidi binafsi katika uchaguzi huo, akitumia zaidi ya TSh trilioni 1.1 kuunga mkono wagombea wa Republican, huku sehemu kubwa ya fedha hizo zikielekezwa katika kampeni za majimbo ambayo chama hicho kilikuwa kikitarajia kupata ushindi.

Hata hivyo, jitihada zake hazikuzaa matokeo yaliyotarajiwa katika baadhi ya maeneo muhimu, yakiwemo Texas na Kansas, ambako wagombea wa chama cha Democratic walipata ushindi.

Akizungumzia matokeo hayo, Musk amesema hali hiyo imeonesha kuwa fedha pekee haziwezi kuamua matokeo ya uchaguzi nchini Marekani.

Katika mahojiano hayo, Musk pia ameweka wazi kuwa hajitambulishi kama sehemu ya vuguvugu la MAGA linalohusishwa na Rais Donald Trump, licha ya kuwa na uhusiano wa karibu wa kisiasa na rais huyo.

Amesema haungi mkono kila msimamo wa chama cha Republican na kwamba anaamini vyama vyote viwili vikuu nchini Marekani vina mazuri na mapungufu yake.

Kauli hiyo inatofautiana na msimamo wake wa awali, ambapo aliwahi kutumia jina la ‘Dark MAGA’ wakati akishiriki kampeni za kumuunga mkono Trump.

Katika hatua nyingine, Musk ameonesha matumaini ya kuwa na uhusiano mzuri wa kikazi na gavana mteule wa Texas, Gina Hinojosa, ambaye amewahi kumkosoa bilionea huyo.

Musk amesema anaamini Hinojosa anaweza kuwa kiongozi mwenye msimamo wa wastani kisiasa na kwamba hatarajii kuwepo kwa matatizo katika shughuli za kampuni zake za Tesla na SpaceX ambazo zina uwekezaji mkubwa katika jimbo hilo.

Amesema kutokana na taarifa alizonazo kuhusu Hinojosa, anaamini kutakuwa na mazingira mazuri ya kushirikiana na serikali yake.

Leave a Comment