×

Mauaji ya Wanawake Yatikisa Afrika Kusini, 581 Wauawa

Takriban wanawake 581 wameuawa nchini Afrika Kusini katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia Julai hadi Septemba mwaka huu, kwa mujibu wa takwimu mpya za uhalifu zilizotolewa nchini humo.

Takwimu hizo zimeibua wasiwasi kuhusu ongezeko la ukatili dhidi ya wanawake, huku jimbo la Gauteng, linalojumuisha mji wa Johannesburg, likiongoza kwa kuwa na wanawake 131 waliouawa katika kipindi hicho.

Miongoni mwa matukio yaliyozua hasira kubwa nchini humo ni kupatikana kwa miili ya wanawake 13 ikiwa na majeraha katika maeneo mbalimbali karibu na Johannesburg, hali iliyosababisha wananchi kuitaka serikali na vyombo vya usalama kuchukua hatua za haraka kuwabaini waliohusika.

Aidha, katika tukio jingine la kusikitisha lililoripotiwa mapema wiki hii katika jimbo la Free State, wanawake watano pamoja na mtoto mmoja mdogo waliuawa kwa kupigwa risasi.

Matukio hayo yameongeza shinikizo kwa polisi kuhakikisha wanafanya uchunguzi wa kina na kuwafikisha mbele ya sheria wote wanaohusika na mauaji hayo.

Afrika Kusini imeendelea kukabiliwa na changamoto kubwa ya ukatili wa kijinsia na mauaji ya wanawake, huku takwimu hizo mpya zikionyesha ukubwa wa tatizo na haja ya kuimarisha hatua za kulinda usalama wa wanawake na watoto.

Hali hiyo imeendelea kuibua wito wa kuchukuliwa kwa hatua madhubuti katika kupambana na ukatili wa kijinsia na kuhakikisha wahusika wanawajibishwa kwa mujibu wa sheria.

Leave a Comment