×

Mwigulu Atoa Onyo kwa Viongozi Wanaojiigawia Vizimba, Aagiza Wapewe Wafanyabiashara Mlandizi

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, ametoa onyo kwa viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha dhidi ya tabia ya kujigawia vizimba vya biashara katika masoko yanayojengwa na Serikali na kisha kuwakodishia wafanyabiashara kwa gharama kubwa.

Dkt. Mwigulu amesisitiza kuwa vizimba vya Soko la Kisasa la Mlandizi vinapaswa kugawiwa moja kwa moja kwa wafanyabiashara watakaovitumia kufanya shughuli zao, badala ya kupitishwa kwa watu wanaolenga kuvipangisha na kupata faida.

 

Ametoa maelekezo hayo Novemba 21, 2026, wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Viwanja vya Shule ya Msingi Mtongani, wilayani Kibaha, mkoani Pwani, baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa soko hilo.

“Vizimba hivi wapewe watu wanaofanya biashara wao wenyewe,” amesema Dkt. Mwigulu, akionya viongozi dhidi ya kujichukulia maeneo ya biashara yanayojengwa kwa gharama za Serikali.

Aidha, Waziri Mkuu ameitaka Halmashauri kuhakikisha ushuru unaotozwa kwa wafanyabiashara watakaoanza kutumia soko hilo unakuwa mdogo katika hatua za awali, ili kuwapa nafasi ya kukuza biashara zao, kupata wateja na kuimarisha mitaji yao.

Amesema ushuru mkubwa tangu mwanzo unaweza kuwa kikwazo kwa wafanyabiashara wadogo ambao wanahitaji muda wa kuzoea mazingira mapya ya biashara na kujenga wigo wa wateja.

Katika hatua nyingine, Dkt. Mwigulu ameagiza ujenzi wa Soko la Kisasa la Mlandizi, unaogharimu Shilingi bilioni 7.71, ukamilike ifikapo Desemba mwaka huu ili wafanyabiashara waweze kuhamia katika eneo hilo na kuendelea na shughuli zao.

Ameeleza kuwa kukamilika kwa soko hilo ni muhimu kutokana na mipango ya ujenzi wa barabara kubwa inayotarajiwa kupita Mlandizi, ambapo baadhi ya maeneo yanayotumiwa sasa na wafanyabiashara yatahitaji kupisha utekelezaji wa mradi huo wa miundombinu.

Awali, wakati akikagua mradi huo, Waziri Mkuu alihoji muundo wa vizimba 770 vilivyojengwa katika soko hilo, ambavyo vinafanana kwa ukubwa na usanifu, akitaka kufahamu namna vitakavyokidhi mahitaji ya wafanyabiashara wanaouza bidhaa za aina mbalimbali.

Maelekezo hayo yanalenga kuhakikisha soko hilo linapokamilika linakuwa na mfumo wa ugawaji wa maeneo uliozingatia mahitaji ya wafanyabiashara, pamoja na gharama zinazowawezesha kuendesha shughuli zao bila kukabiliwa na changamoto zisizo za lazima.

Leave a Comment