
Mwandishi wa habari wa Global Publishers, Richard Bukos, ametunukiwa Stashahada ya Uandishi wa Habari katika mahafali ya tatu ya Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam yaliyofanyika leo.
Akizungumza mara baada ya kutunukiwa stashahada hiyo, Bukos ameeleza furaha yake na kutoa shukrani za dhati kwa uongozi pamoja na wafanyakazi wa Global Publishers kwa mchango wao mkubwa katika kumwezesha kufikia mafanikio hayo ya kitaaluma.

Amesema mafanikio hayo yatabaki kuwa sehemu ya kumbukumbu muhimu katika maisha yake, akitambua namna kampuni hiyo ilivyomsaidia kwa hali na mali katika safari yake ya elimu.
“Ukweli, tangu nilipojiunga na Global pamekuwa ni sehemu ya familia yangu kutokana na ushirikiano mkubwa wa kifamilia ninaoupata, hata katika masuala binafsi,” amesema Bukos.
Aidha, ametoa shukrani za pekee kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Global Publishers, Eric Shigongo, kwa kuendelea kuwa naye bega kwa bega tangu mwaka 2006 walipoanza safari yao ya pamoja wakiwa Kariakoo.

Pia, namshukuru Meneja Mkuu, Abdallah Mrisho na viongozi wengine wote pamoja na wafanyakazi wenzangu wote kwa mchango wao mkubwa katika kufanikisha hatua hii ya maisha yangu.
Mafanikio ya Bukos ni sehemu ya safari yake ya kujiendeleza kitaaluma huku akiendelea na majukumu yake ya uandishi wa habari katika kampuni ya Global Publishers.
Hongera sana Richard Bukos kwa hatua hii muhimu! Elimu ni safari isiyo na mwisho.