×

Album ya 911 Yazua Moto! Zuchu na Nandy Watupiana Maneno

Msanii wa Bongo Fleva, Bongo Fleva, Zuhura Othman maarufu Zuchu.

MSANII wa Bongo Fleva, Zuhura Othman maarufu Zuchu, ameendelea kuweka wazi malalamiko yake dhidi ya msanii mwenzake, Faustina Mfinanga almaarufu Nandy, akifichua madai mbalimbali ya matukio yaliyodaiwa kuchangia kutokuelewana kwao, huku akimtaka Nandy amfuate ana kwa ana ikiwa anataka kuendeleza bifu hilo.

Kupitia ujumbe aliouandika, Zuchu amedai kuwa Nandy aliwahi kumtumia stylist wake kwa ajili ya kuiga baadhi ya mitindo yake ya urembo, ikiwemo nywele, huku akieleza kuwa amekuwa akikutana na matukio mbalimbali ambayo hakupenda kuyaweka hadharani ili kuepusha migogoro.

Aidha, Zuchu amezungumzia suala la aliyekuwa meneja wake, Doris, akidai kuwa baada ya kumwondoa kwenye nafasi hiyo, Nandy alikutana naye na kuanza kuhusishwa naye katika mazingira ambayo Zuchu ameyatafsiri kama kutafuta namna ya kumkera.

Katika hatua nyingine, Zuchu amedai kuwa aliwahi kupewa ushauri kuhusu mtu aliyekuwa akimtengenezea nywele, lakini baadaye alipoona ukaribu wa watu hao, aliamua kujiondoa ili kuepusha malumbano.

Zuchu pia amegusia suala la matangazo ya matukio, akidai kuwa baada ya yeye kutangaza shughuli yake ya Imbeju, Nandy naye alitangaza tamasha, jambo ambalo amelihusisha na ushindani kati yao.

Ameongeza kuwa amekuwa akivumilia mambo mengi bila kuyazungumza hadharani, huku akidai kuwa kuna watu waliokuwa wakimzungumzia kuhusu kutopata dili la pombe licha ya madai yake kuwa suala hilo lilikuwa limekwishughulikiwa.

Staa wa kike wa Bongo Fleva, Faustina Mfinanga almaarufu Nandy.

Katika ujumbe huo, Zuchu amesema hataki kuendelea na mizunguko ya maneno na badala yake amemtaka Nandy, ikiwa ana jambo naye, amfuate ana kwa ana.

“Sasa ukiwa unataka bifu niletee usoni, hivi sisi watu wazima punguza mizunguko,” ameandika Zuchu.

Hata hivyo, Nandy naye amevunja ukimya na kumjibu Zuchu kufuatia ujumbe huo, akihusisha malalamiko hayo na maandalizi ya albamu yake mpya inayotarajiwa kutoka Novemba 27, yenye jina la 911.

Kupitia ujumbe wake, Nandy ameandika: “Yaani da Zuu nimeweka tracklist tu umefanya media tour… Zikitoka nyimbo si utaufa?🤣🤣😂😂”

Majibizano hayo yameibua mjadala miongoni mwa mashabiki wa muziki wa Bongo Fleva, huku macho na masikio yakielekezwa kwenye albamu ya Nandy pamoja na hatma ya tofauti zinazodaiwa kuwepo kati ya wasanii hao wawili.

>

Leave a Comment