×

Rasmi! Ruto, Tshisekedi Wakubali Kurejesha Uhusiano wa Kidiplomasia

Rais wa Kenya, William Ruto, na mwenzake wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Félix Tshisekedi, wamekubaliana kurejesha uhusiano wa kidiplomasia na kuimarisha ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili.

Makubaliano hayo yalifikiwa jana Novemba 22, 2026 katika Mkutano wa Kisiasa wa Ngazi ya Juu wa Nchi Nne uliofanyika mjini Oyo, Jamhuri ya Congo.

Mkutano huo uliongozwa na Rais Denis Sassou N’Guesso wa Jamhuri ya Congo, huku Rais wa Baraza la Mawaziri la Togo, Faure Essozimna Gnassingbé, ambaye pia ni mpatanishi wa Umoja wa Afrika katika mzozo wa mashariki mwa DRC, akihudumu kama mpatanishi.

Katika makubaliano hayo, Ruto na Tshisekedi wamekubaliana kurejesha uwakilishi wa kidiplomasia wa nchi zao katika ngazi ya mabalozi, kuanzisha tena mashauriano ya mara kwa mara ya kisiasa pamoja na kuendeleza shughuli za Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Kenya na DRC.

Aidha, viongozi hao wameahidi kuimarisha ushirikiano katika masuala ya amani na usalama wa kikanda, hususan katika kukabiliana na changamoto zinazohusu eneo la Maziwa Makuu.

Pia wameeleza dhamira ya kuimarisha ushirikiano kupitia taasisi za kikanda, zikiwemo Mkutano wa Kimataifa wa Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Makubaliano hayo yanaashiria hatua ya kurejesha mawasiliano ya kidiplomasia kati ya Kenya na DRC, huku ushirikiano wa kikanda ukiendelea kuwa sehemu muhimu ya juhudi za kukuza amani, usalama na maendeleo katika eneo la Maziwa Makuu.

Leave a Comment