
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amezitaka tume za uchaguzi za nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kutumia ipasavyo teknolojia za kisasa, mitandao ya kijamii na akili unde (AI) katika kuboresha usimamizi wa uchaguzi na kuimarisha demokrasia katika ukanda huo.
Dkt. Mwigulu amesema teknolojia hizo zina nafasi muhimu katika kurahisisha mawasiliano, kutoa elimu kwa wapiga kura na kuhakikisha wananchi wanapata taarifa sahihi kuhusu michakato ya uchaguzi kwa wakati.

Hata hivyo, amesisitiza kuwa pamoja na fursa zinazotokana na matumizi ya teknolojia hizo, tume za uchaguzi zinapaswa kuweka mikakati madhubuti ya kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza, hususan usambazaji wa taarifa potofu zinazoweza kuathiri amani, mshikamano wa jamii na imani ya wananchi katika taasisi za uchaguzi.
Amesema taarifa zisizo sahihi zinaposambazwa kwa kasi wakati wa uchaguzi zinaweza kusababisha migawanyiko katika jamii, kuathiri taswira ya taasisi za uchaguzi na kupunguza imani ya wananchi katika michakato ya kidemokrasia.

Waziri Mkuu ametoa wito huo leo, Jumatatu, Novemba 23, 2026, wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 28 wa Jukwaa la Tume za Uchaguzi za Nchi Wanachama wa SADC (ECF-SADC), unaofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency – The Kilimanjaro, jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo wa siku tatu unajadili usimamizi wa uchaguzi katika zama za mitandao ya kijamii pamoja na namna ya kuimarisha wajibu wa taasisi za usimamizi wa uchaguzi katika ukanda wa SADC.
Akizungumzia nafasi ya mitandao ya kijamii, Dkt. Mwigulu amesema imekuwa chanzo muhimu cha taarifa kwa wananchi wengi, hususan vijana, kutokana na uwezo wake wa kusambaza habari kwa haraka na kufikia watu wengi kwa muda mfupi.

Aidha, amezitaka tume za uchaguzi kuendelea kujenga uwezo wa kitaalamu katika matumizi ya akili unde, akibainisha kuwa teknolojia hiyo inakua na kubadilika kwa kasi, hivyo ni muhimu kwa taasisi hizo kujiandaa kukabiliana na changamoto zake huku zikitumia fursa zinazotokana na maendeleo yake.
Amesisitiza kuwa matumizi ya AI yanapaswa kuambatana na mikakati inayozingatia mazingira ya uchaguzi, ili kuhakikisha teknolojia hiyo inachangia kuboresha utendaji wa tume na kuimarisha upatikanaji wa taarifa kwa wananchi.
Dkt. Mwigulu amehimiza nchi wanachama wa SADC kuimarisha uwezo wa taasisi zao za uchaguzi katika kukabiliana na mabadiliko ya teknolojia, ili kulinda uaminifu wa michakato ya uchaguzi na kuendeleza misingi ya demokrasia katika ukanda huo.