×

China Yatua Kenya na Teknolojia ya AI! Wanahabari Kuingia Kwenye Mapinduzi ya Kidijitali

NAIROBI, KENYA– Ushirikiano wa kiteknolojia kati ya China na Afrika umechukua hatua nyingine baada ya China kuzindua programu maalumu ya mafunzo ya matumizi ya Akili Bandia (AI) kwa wanahabari nchini Kenya, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuimarisha uwezo wa vyombo vya habari katika kukabiliana na mabadiliko ya kidijitali.

Mafunzo hayo ya siku mbili yalianza jijini Nairobi jana, Novemba 24, 2026, yakilenga kuwajengea uwezo wataalamu wa sekta ya habari katika matumizi ya teknolojia ya AI kwenye uzalishaji, uhariri na uripoti wa habari.

Programu hiyo imeandaliwa na Mamlaka ya Redio na Televisheni ya Kitaifa ya China (NRTA) pamoja na Akademia ya Sayansi ya Utangazaji (ABS), kwa ushirikiano na Ubalozi wa China nchini Kenya na vyombo mbalimbali vya habari vya Kenya.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo, Msaidizi wa Balozi wa China nchini Kenya, Zhang Zhizhong, amesema ushirikiano katika sekta ya habari ni sehemu muhimu ya mahusiano kati ya China na Kenya, huku ukiwa na mchango mkubwa katika kuimarisha uelewano kati ya wananchi wa mataifa hayo mawili.

Amesema mafunzo hayo ni utekelezaji wa vitendo wa Mpango wa Ushirikiano wa China na Afrika kuhusu Redio, Televisheni na Ubunifu wa Sauti na Picha, uliotangazwa katika Mkutano wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika Beijing mwaka 2024.

Kwa upande wake, Mshauri wa Ngazi ya Kwanza katika Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa ya NRTA, Shi Zhiyan, amesema mpango huo unalenga zaidi ya kuwafundisha wanahabari matumizi ya AI, bali pia kuwapa uelewa wa kina kuhusu teknolojia hiyo na fursa zinazoweza kuleta katika sekta ya habari.

Ameeleza kuwa kupitia mafunzo hayo, wanahabari wa Kenya watapata nafasi ya kuongeza ujuzi wao wa kiteknolojia, kuboresha namna ya kusimulia habari za Afrika na kuhakikisha sauti za bara hilo zinapata nafasi katika maendeleo ya teknolojia ya akili bandia.

Hatua hiyo inakuja wakati matumizi ya AI yakizidi kuleta mabadiliko katika tasnia ya habari duniani, ikiwemo namna habari zinavyotafutwa, kuchambuliwa, kuandaliwa na kusambazwa kwa hadhira.

Kupitia ushirikiano huo, China na Kenya zinatarajia kuimarisha zaidi uhusiano wa vyombo vya habari na kukuza uwezo wa wataalamu wa Afrika kutumia teknolojia mpya katika mazingira ya kazi yanayobadilika kwa kasi.

Leave a Comment