
DAR ES SALAAM, Tanzania – Kampuni ya Coca-Cola imetangaza kurejea katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) baada ya takribani miaka 30, kufuatia makubaliano mapya ya ushirikiano na Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF), yatakayoifanya kampuni hiyo kuwa mdhamini rasmi wa michuano ya TotalEnergies CAF AFCON 2027.
Michuano hiyo inatarajiwa kufanyika Afrika Mashariki mwaka 2027, huku ushirikiano huo ukilenga kuimarisha uhusiano kati ya soka, burudani na tamaduni za mashabiki wa mchezo huo barani Afrika.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ushirikiano huo unaashiria ukurasa mpya katika historia ya Coca-Cola na soka la Afrika, huku kampuni hiyo ikirejea katika mashindano ambayo imewahi kuwa sehemu ya wadhamini wake miaka iliyopita.
Coca-Cola imeeleza kuwa soka la Afrika lina nafasi kubwa katika kuunganisha watu, jamii na mataifa mbalimbali, si kupitia matukio yanayotokea viwanjani pekee, bali pia kupitia tamaduni, nyimbo, burudani na shauku ya mashabiki.
Kupitia ushirikiano huo, kampuni hiyo inalenga kusherehekea mchango wa mashabiki na jamii mbalimbali zinazofanya AFCON kuwa moja ya mashindano yenye mvuto mkubwa barani Afrika.
Akizungumzia ushirikiano huo, Rais wa Kitengo cha Uendeshaji cha Coca-Cola barani Afrika, Luis Felipe Avellar, amesema kampuni hiyo inajivunia kuungana tena na CAF na kushiriki katika mashindano yenye nafasi ya kipekee kwa Waafrika.
Amesema Coca-Cola inatarajia kutumia fursa hiyo kusherehekea mashabiki na jamii zinazochangia kuifanya soka kuwa sehemu muhimu ya maisha ya watu barani humo.
Kwa upande wake, Rais wa CAF, Dkt. Patrice Motsepe, amesema shirikisho hilo linafurahi kuikaribisha tena Coca-Cola katika soka la Afrika baada ya takribani miaka 30.
Motsepe ameeleza kuwa ushirikiano huo unatarajiwa kuchangia maendeleo na ukuaji wa soka barani Afrika, pamoja na kuimarisha maslahi ya kibiashara kwa wadau wa pande zote mbili.
Aidha, amesema imani inayooneshwa na wadhamini na wawekezaji wa ndani na nje ya Afrika inaonesha umuhimu wa mifumo ya utawala, uwazi, maadili na viwango vya biashara vinavyotekelezwa na CAF.
Ushirikiano huo unakuja wakati ambapo Afrika Mashariki inajiandaa kuwa mwenyeji wa michuano ya AFCON 2027, ambayo inatarajiwa kuleta pamoja mashabiki kutoka mataifa mbalimbali na kutoa fursa ya kuonesha uwezo wa ukanda huo katika kuandaa mashindano makubwa ya soka.
Mashabiki wanahimizwa kufuatilia kurasa rasmi za Coca-Cola na CAF kwenye mitandao ya kijamii ili kupata taarifa zaidi kuhusu ushirikiano huo na maandalizi ya AFCON 2027.