×

Usipige Bwana…Tuma Meseji!-12

ILIPOISHIA GAZETI LA IJUMAA WIKIENDA:
“Vipi tena shem?” Nancy alimuuliza Bony  baada ya kumwona akifika kwenye meza yake na kukaa huku uso wake ukikosa uchangamfu ule anaoujua yeye…
“Du! Shem, umenishtua sana kusema umeshaongea na Neema, ikabidi nije nijue umeongea naye kuhusu nini hasa? Kwamba tumekutana hapa? Kwamba niko na demu au kwamba nini?” Bony aliuliza huku akijua amani yake iko kwenye majibu ya Nancy kuhusu hicho alichoongea na Neema…
TAMBAA NAYO MWENYEWE…


Kwani shem wewe una wasiwasi gani mimi nikiongea na Neema wakati unajua ni rafiki yangu kipenzi na ni matroni wake?” alisema Nancy huku akijua kuwa, Bony yupo na mchepuko ndiyo maana ameonekana kushtuka sana…
“Hakuna ubaya shemu…ila unajua kama vile tena, umeniona niko na yule dada, sasa kama umemwambia Neema kwamba umeniona na demu, atamaindi sana shemu…”
“Kumbe shem unachepuka ee?” Nancy alihoji kwa ukali…
“Hapana shem, ila…”
“Mmm! Shemeji! Kama huchepuki kwa nini unaogopa Neema kujua upo na mwanamke, tena mwanamke mwenyewe mrembo!”
Bony aliangalia chini kwa aibu kwani ukweli aliujua na alichokuwa akitetea yeye ni kama Neema ameambiwa mwanamke mwenyewe alivyovaa, atajua ni Aisha, nini kitatokea wakati alishaanza kuonesha shaka kwa mbaaali sana…
“Lakini shem mimi nakushangaa sana, mimi niko na Neema miaka mingi, hakuna hata siku moja umewahi kunitamkia neno la mapenzi. Je, unataka kuniambia sivutii? Sina sifa ya kuwa mwanamke mrembo..?
“Je, huyu uliyepita naye hapa shemeji na mimi ni nani zaidi kwa uzuri? Kuwa mkweli shemeji…”
“Wewe shemeji!”
“Sasa kwa nini hata siku moja hujawahi kunitamkia kwamba una hisia na mimi shemeji?”
“Da! Shemeji…kwani wewe una hisia na mimi?” Bony alimuuliza Nancy…
“Sana tu shemeji,” Nancy alijilipua.

Moyoni Bony akajua presha yake imepotea kiulaini kama Nancy anahisia na yeye kama ilivyokuwa kwa Aisha…
“Nimekuelewa sana shemeji, hilo tufanye limeisha kabisa…”
“Limeishaje shemeji?” aliuliza Nancy akimwangalia Bony kwa macho ya mlegezo…
“Nimekuelewa kwamba, kumbe ulikuwa una hisia na mimi ila hukuwahi kuniambia tu.”
“Sasa limeishaje?”
“Hata mimi nina hisia na wewe.”
“Lini sasa tunakutana?”
“Wewe tu.”
“Lakini nikisema leo si tayari upo na yule bibie pale?”
“Yule anaweza kuondoka zake muda wowote ule.”
“Mm! Kweli shemeji? Isijekuwa nakukata stimu zako?”
“Hamna, hunikati stimu yoyote ile.”
“Basi mimi nipo sana hapa kwa ajili yako shemeji. Nashukuru  leo nimetoa dukuduku langu kuhusu wewe na umenielewa,” alisema Nancy akianza kuona aibu kwani kwa mwanamke kujianika vile si rahisi labda awe mkongwe wa matukio.
Bony alirejea kwa Aisha akiwa na furaha moyoni lakini hakutaka kuionesha waziwazi ili Aisha asijue…
“Anasemaje?”
“Mpuuzi yule, si amemwambia amekutana na mimi hapa lakini hakumwambia niko na wewe. Sasa Neema akamwambia anakuja muda wowote ili ale chakula cha jioni hapahapa,” Bony alidanganya…
“He! Kwa hiyo sasa mimi si niondoke?”
“Itabidi iwe hivyo sweet.”
Aisha hakutaka kupoteza hata dakika moja, alisimama, akabeba mkoba wake na kuondoka.

Wakati anapita jirani na meza aliyokaa Nancy, alimwangalia, wakakutana macho, Aisha akabinua midomo, Nancy akaachia tabasamu la kejeli.
***
Bony alijishika kichwa akiyafikiria maneno mazito kutoka kwenye kinywa cha Nancy.
Ilivyo ni kwamba, hata wakati anafunga ndoa, Bony aliwahi kumnong’oneza rafiki yake mmoja anaitwa Delima akimwambia kwamba, matroni wa Neema, yaani Nancy ni mzuri sana kuliko bibi harusi…
“Delima, umemcheki matroni lakini. Amefunga, amejazia kila idara. Mtoto ameumbwa kama kapita kwenye kiwanda cha magari,” Bony alimwambia Delima…
“Sijui ni kwa nini? Unajua maharusi wengi, mamatroni ndiyo wazuri kuliko mabibi harusi,” alijibu Delima.”
Sasa siku hiyo kutokea Nancy ndiye anaomba hisia zake zitambulike, Bony alihisi amepata muujiza ambao hakuwahi kuufikiria.

Mara simu yake iliita, alipiga Neema…
Je, nini kiliendelea hapo? Usikose kusoma chombezo hili jipya kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda, Jumatatu ijayo.

Leave a Comment