×

Nilivunja Ndoa Yangu na Shetani-24

ILIPOISHIA:
“Konsooo, kwa vile upo na mimi nitakutumia kutengeneza pesa ambazo hukuwahi kuziota ndotoni.”
Makubwa nilijikuta njia panda juu ya kauli ya Papaa kuwa ndani ya mwaka mmoja nitakuwa tajiri mkubwa mwenye kanisa langu huku nikitenda miujiza itakayoitikisa dunia. Bado kwangu niliona mauzauza kutokana na kauli yake juu ya ucha Mungu wake na matendo yake kwenda tofauti.
SASA ENDELEA…

“Papaa mbona unanipa matumaini ya ndotoni?”
“Tangu ufike hapa umeona kitu gani cha gharama ya chini?” aliniuliza kuhusu utajiri wake.
“Sijaona.”
“Basi ndani ya mwaka nawe utakuwa na nyumba zaidi yangu na pesa nyingi tu.”
“Mmh! Sawa,” nilimkubalia ili tulimalize lakini niliona ananidanganya uongo wa kitoto.
“Kwa leo huwezi amini ila kuanzia leo utaona maisha yako yanabadilika, kwa kazi ambayo utaifanya baada ya wiki tatu, miezi mitatu baadaye tunafunga ndoa ya kifahari.”
“Unataka niwe mkeo?” nilishtuka kidogo.

“Ndiyo, wewe si mwanamke wa kuumwa na mbu na kupigwa baridi unatakiwa uwe chini ya watu wenye pesa kama sisi.”
“Mmh! Makubwa, kazi gani mbona unanitisha?”
“Ya kawaida ukiifanya vizuri malipo yake ni milioni kumi na tano (pesa za Kitanzania).”
“Ni kazi gani hiyo? Ya kubeba unga?” niliuliza japo akili yangu ilikuwa tayari kwa kazi yoyote ya kuniingizia pesa.
“Wala siwezi kufanya biashara kama hiyo hata siku moja.”
“Sasa hiyo biashara gani?”
“Ya kutangaza dini.”
“Mmh! Nitaitangazaje dini niwe tajiri?”
“Sikiliza Konso, japokuwa sikufahamu vizuri sina budi kukueleza sababu ya kukutafuta wewe ili tufanye kazi ambayo ina sura mbili.”
“Sura mbili una maana gani?”
“Sura ya mbele huonesha wacha Mungu waliomshika Bwana, lakini sura ya ndani ni utapeli wa kutumia neno lake kujiingizia pesa.”
“He! Makubwa, sasa kwa nini mnafanya hivyo?”
“Konso, umetoka Tanzania kuja Kenya kufanya biashara ya kujidhalilisha ili kupata pesa, biashara ambayo ni chukizo mbele ya Mungu.”
“Sawa, lakini kazi yangu ipo wazi na mtu ana hiyari ya kufanya mapenzi na mimi  au kuacha wala simlazimishi, tofauti na ninyi kutumia kivuli cha ucha Mungu kutenda maovu.”
“Konso anayeuza mwili na tapeli nani mwenye afadhali?”
“Mmh! Afadhali anayeuza mwili kwa vile tapeli akishikwa anaweza kuuawa kwa kupigwa na mwisho kuchomwa moto na kufa kifo kibaya.”
“Konso ipi dhambi kubwa ya utapeli na uzinzi?”
“Zote dhambi.”
“Siku zote ukitaka kula nguruwe kula aliyenona, fanya dhambi hata ukihukumiwa basi kweli liwe kosa. Hii siri nimekueleza wewe tu hakuna hata mmoja anayeijua kuwa sitangazi Neno la Mungu bali kutafuta pesa japokuwa nimewasaidia wengi sana wenye mikosi, ugumba na waliokata tamaa ya maisha wote walifanikiwa.

“Konso ukinikuta kazini mimi ni mtu mwingine, kanisa langu linajaza kupindukia na kila anayefika pale anajua mimi ni nani. Jina langu kubwa, naingia ikulu kama kwangu.”
“Mmh! Sasa kama unasaidia wenye shida utapeli wako upo wapi?”
“Tukimaliza kazi nitakayokupa utajua kila kitu, nitakushirikisha rasmi kwenye utengenezaji wa pesa wenye siri kubwa nyuma ya pazia. Hata Bwana Yesu alisema siyo wote wanaoniita bwana bwana wataingia katika ufalme wa mbinguni.”
“Mmh! Makubwa.”
“Sasa ni hivi, hii siri ninayokupa nikiisikia popote ujue utakuwa umeuza uhai wako.”
“He! Makubwa kama hivyo basi sihitaji kuifanya hiyo kazi,” niliamua kuikataa baada ya kutishiwa kifo.
“Kwa vile umeishajua baadhi ya mambo yangu lazima utaifanya kwa hiyari au kwa nguvu,” Papaa ghafla alinigeuka na kusema kwa sauti ya ukali.
“Lakini hii kazi sikuitaka miye.”
“Konso hiki ni kiapo ukienda kinyume lazima ufe.”
“Unataka kuniambia wapo waliotangulia walifanya makosa wakafa.”
“Ndiyo.”
“Wangapi?”
“Hiyo siyo juu yako, kama nilivyokueleza ukiifanya kazi vizuri utaishi kama peponi lakini ukinizingua ni sekunde kuwa mgeni wa kuzimu.”
“Papaa kwa nini unaniingiza kwenye kazi bila ridhaa yangu?” woga uliniingia.

“Hii kazi ni nyepesi kuliko kuuza mwili, kazi ya kuuza mwili unaweza kupata magonjwa na kufa au biashara yako ikafa. Lakini kazi hii ni hesabu tu ambazo huwa hazikatai kwa vile tayari nimeisha jenga msingi imara.”
“Sawa, ni kazi gani?”
“Kama nilivyokueleza kazi yangu ina sura mbili, kuna kitu tunataka kukifanya ili kuwaziba watu macho hata ukiwa msaidizi wangu basi watu wawe na ushuhuda wa kweli.”
“Sawa, nieleze hiyo kazi.”
“Kanisa langu limepata sifa nyingi kutenda miujiza ambayo mingi huwa ya kutengeneza kama huu nitakao utengeneza kwako.”
“Huo muujiza upi?”
Je, kitafuatia nini? Usikose Gazeti la Risasi Mchanganyiko siku ya Jumatano.

Leave a Comment