ILIPOISHIA ILIYOPITA:
Mkoba wangu nilikuwa nimeuacha kule chumbani. Nikatoka nje ya ile hoteli. Nilipotupa macho, nikaliona gari la Eddy likiwa limeegeshwa katika eneo la kuegesha magari. Nikalifuata. Nilimkuta Eddy amelalia usukani wa gari.
Nikafungua mlango wa dereva na kumuita.
“Eddy!”
Wakati mlango unafunguka nikamuona Eddy anachomoka kwenye mlango na kuanguka chini kama mzigo. Nikawahi kumdaka.
Alikuwa ametoa macho na damu ilikuwa ikimtoka puani na midomoni.
SASA ENDELEA…
“Eddy! Eddy! Una nini?” nikamuuliza nikiwa nimemshikilia.
Lakini Eddy alikuwa amelegea mwili mzima. Shingo yake ilikuwa imelegea kama iliyovunjwa.
Ilikuwa hali iliyonishtua sana na kunipotezea nguvu zangu zote. Mwili wa Eddy ulinielemea, nikauachia ukaanguka chini kama mzigo. Vile alivyoanguka ndivyo alivyolala hivyohivyo. Baada ya kuutazama uso wake mara moja niligundua kuwa Eddy hakuwa hai. Alikuwa ameshakufa!
Nilitaka nichutame ili nimchunguze vizuri lakini nikamuona mlinzi wa hoteli aliyekuwa ameketi mbali kidogo karibu na lango la kuingilia hotelini akinyanyuka.
“Kuna nini hapo?” akapaza sauti kuniuliza.
Alikuwa amekiona kile kitendo kilichotokea pale cha Eddy kuanguka chini kutoka kwenye gari lake huku na mimi nikionekana nimechanganyikiwa.
Nikajiuliza nitamueleza nini kuhusu hali ya Eddy wakati sijui kilichomtokea na wakati huohuo mimi ndiye niliyeonekana naye hapo? Nikaamua kuondoka haraka.
Mlinzi naye akanifuata. Alikuwa anakuja kwa upande wangu wa kushoto, mimi niliondoka kwa upande wa kulia.
Simu yangu ilikuwa mkononi lakini mkoba wangu niliuacha kule chumbani juu ya kitanda. Kwa vyovyote vile nisingeweza kuingia tena katika hoteli hiyo. Si kwa sababu nilitaka kumkimbia yule mlinzi bali pia kule chumbani kulikuwa na yule jini.
Huku nikizibwa na magari yaliyokuwa yameegeshwa, niliendelea kwenda huku nikitazama nyuma mara mojamoja. Sikuweza kumuona tena yule mlinzi kwa sababu alizibwa na magari na yeye hakuwa akiniona. Nikatokomea!
Kusema kweli nilikuwa natembea huku nimechanganyikiwa. Nilikuwa sijui naenda wapi. Nilikuwa nimeshalitoka eneo lile la hoteli na kuingia katika mtaa mwingine.
“Hili ni balaa!” nilijiambia kimoyomoyo.
Nilishindwa kugundua nini kilikuwa kimetokea. Yule mzungu alifikaje katika chumba cha Eddy wakati Eddy mwenyewe akiwa kwenye gari? Au kitu gani kimemtokea Eddy?
Kwa vyovyote vile, nilijiambia, chochote kile kilichomtokea Eddy kimetokana na yule jini.
“Kama Eddy atakuwa ameuawa, ameuawa na yule jini? Nikajiambia.
Na amemuua baada ya kuona alikuwa mpenzi wangu na nilikuja Unguja kumfuata yeye. Siku ile ya kwanza nilipokutana naye nilimwambia kwamba sikuwa na mpenzi wala mchumba.
Sasa ameamua kunikomoa!
Kutokana na damu iliyokuwa inamtoka Eddy puani na midomoni huenda alikabwa shingo au shingo yake ilinyongwa na kuvunjwa kabisa. Au, niliendelea kujiambia. Eddy atakuwa amefyonzwa damu na yule jini.
Akili yangu iliniambia kwamba yule mlinzi anaweza kuufahamisha uongozi wa hoteli kuhusu kifo cha Eddy. Na uongozi huo ukapiga simu polisi.
Polisi watakapofika mlinzi atasema alimuona msichana aliyeuangusha mwili huo na kukimbia. Hapo ni wazi kuwa mtuhumiwa nitakuwa mimi na polisi wataanza kunitafuta.
Kama itakuwa hivyo, niliendelea kujiambia, jambo la maana ni kuondoka pale Unguja haraka. lakini nikakumbuka kwamba pochi yangu iliyokuwa na pesa niliiacha kule chumbani. Pale nilipokuwa sikuwa hata na senti tano!
“Nitapata wapi pesa ya nauli ya kunirudisha Dar?” nikajiuliza bila kupata jibu.
Pale Unguja sikuwa na mwenyeji yeyote zaidi ya Eddy mwenyewe. Nilianza kufika Unguja baada ya kuwa na uhusiano na Eddy na tulikuwa tukikutana hotelini, hakuwahi kunipeleka nyumbani kwao hata siku moja.
“Sasa nitakwenda kumuomba nani pesa?” nikaendelea kujiuliza.
Nilipofika pale Unguja nilikuwa nikisikia baridi lakini muda ule niliokuwa nimetahayari nilihisi joto limepamba moto kiasi kwamba mwili wangu ulianza kutota jasho. Sikuwa hata na kitambaa cha kujifuta jasho usoni. Kitambaa changu kilikuwa ndani ya mkoba wangu.
Licha ya kutembea kwa mwendo wa haraka nilikielekea bandarini nilijua kuwa wakati wowote ningeweza kukamatwa na polisi. Kwa vile sikuwa na uzoefu wa kutenda vitendo vya uhalifu, kila nilipokutana na polisi nilijishtukia. Polisi yeyote mwenye saikolojia angeweza kugundua kuwa nilikuwa na hisi ya hatia.
Sasa mawazo yangu yote yakawa kwenye kufungwa. Nilijiambia penzi langu na Eddy sasa linanipeleka jela!
Wakati ule mawazo yangu yanatangatanga nikapata wazo la kumpigia simu dada yangu nimueleze yaliyonikuta.
Itaendelea katika Gazeti la Ijumaa siku ya Ijumaa.