×

Matatizo ya kutoona vizuri-2

Wiki iliyopita nilianza kuelezea tatizo la uoni hafifu linalowakabili watu wengi, leo nitaelezea sababu na matibabu ya uoni hafifu wa macho.

Kufifia kwa nuru ya macho kwaweza kuwa dalili ya ugonjwa unaoitwa mayopia, yaani macho kuweza kuona karibu tu, pamoja na makengeza, presha ya macho na maumivu ya kichwa. Myopia ndilo tatizo linalofahamika zaidi ambapo vitu vya mbali hufifia. Miwani, lensi na upasuaji kama vile LASIK na PRK ndizo njia zinazotumika sana kurekebisha tatizo la uoni wa karibu.

Hyperopia (shida ya kuona vitu vya karibu) ni tatizo ambalo vitu vya mbali huonekana kwa macho makali kabisa lakini macho hayo hayo hushindwa kuona vitu vya karibu kabisa, au kuona huko vitu vya karibu husababisha hali isiyo ya kawaida ya msongo na uchovu wa macho. Tatizo hili linapocharuka, hata vitu vya mbali navyo hufifia, tatizo hili nalo laweza kurekebishwa kwa miwani, lensi na upasuaji wa macho.

Astigmatism; Hili ni tatizo la kufifia kwa macho katika masafa yote (karibu au mbali). Mara nyingi husababishwa na umbile lisilo la kawaida la Kornea (Cornea). Kutokana na tatizo hili, miale ya nuru (mwanga) hushindwa kuja katika kituo kimoja cha uoni kwenye retina ili kuleta uoni mzuri, hii haijali kitu kinachoonwa kiko umbali gani. Kama yalivyo matatizo ya kuona karibu na kuona mbali, tatizo hili la Astigmatism nalo laweza kurekebishwa kwa miwani, lensi au upasuaji wa macho.

Presbyopia: Ikiwa umefikisha umri wa miaka 40 na kuendelea, unaanza kupata tatizo la kupoteza nuru ya macho kwa vitu vya karibu kama kushindwa kuona saizi ndogo za herufi za gazeti au maandishi mengine, basi hii ni dalili ya tatizo la Presbyopia ambalo kimaumbile ni tatizo linalojitokeza kwa sababu ya umri.
Tatizo la Presbyopia humuathiri karibu kila mtu anayevuka miaka 45. Watu wengi hutumia miwani ya kusomea au lensi zenye kukuza herufi Bifocal au Progressive Lenses.

Leave a Comment