×

Usipige Bwana…Tuma Meseji!-16

ILIPOISHIA GZETI LA IJUMAA WIKIENDA:
“Siyo kwamba muda umekwenda sana sweet?”
“Noo! Wala, saa hizi muda umekwenda?”
Bony alikubali, akashuka, akamshika mkono Nancy mpaka ndani kwake huku wakiyumbayumba kwa kileo.
SASA JIACHIE MWENYEWE…

Siku hiyo, Nancy alimwomba Bony wasifanye chochote maana yeye alikuwa asimilia 95 kuelekea kwenye ukamilifu baada ya kutoka kwenye rangi nyekundu lakini kesho yake mambo yangekuwa poa kwani angefikia asilimia mia moja ya ukamilifu.
Hata hivyo, Nancy hakutaka kumwacha Bony aondoke hivihivi, alimpa vitu adimu kama vile denda kidogo, mabusu kidogo na kumwangalia kwa kurembua ambako kulimfanya Bony kuhisi joto la mahaba.
Alimwomba akae kidogo, akampa juisi na kunywa kisha akaondoka huku akisindikizwa na mwenyeji wake, Nancy na wakaachana kwa mabusu na baby nyingi.
***
Bony alipofika nyumbani kwake, alipokelewa na macho ya Aisha yakiwa yamejaa hasira na uchungu, Neema hakuwepo, alikuwa chumbani…
“Za saa hizi shemeji?” alisalimia Bony akiwa ameshajua Aisha hakuwa sawasawa…
“Yule malaya wako umemwacha wapi?” aliuliza Aisha huku Neema akitoka chumbani kuja sebuleni…
“Sweethaert, umeniletea maziwa niliyokuagiza?” aliuliza Neema licha ya kwamba alimwona mume wake ameshika mfuko wa ki-supamaketi…
“Ndiyo baby, haya hapa.”
Neema alipokea mzigo huo na kuupeleka kwenye friji, kisha akamwita Bony chumbani…
“Nakuomba mara moja baby.”
Bony alianza kuogopa, alihisi kuna jambo kubwa kwani si kawaida ya mke wake, afike tu na kumwitia chumbani…
“Unajua baby mimi namshangaa sana Aisha,” alianza kusema Neema huku akikaa kitandani…
“Kwa nini sweet?”
“Yaani we unaingia na mfuko yeye anakuangalia tu, hata kusema asimame akupokee, maana yake nini? Ina maana haya ndiyo maisha aliyokuwa akiishi na mumewe Mudy?
“Mbona sisi kwetu hatujalelewa hivyo? Mimi kwetu, baba akija na mzigo mama anasimama kupokea bila kujali watu waliopo…mh! naanza kuhisi mambo mengi kwa Aisha kwamba yatanishinda…”
“Noo Neema, noo! Mungu ametuumba hivyo. Wengine wakamilifu kidogo wengine wako hovyo. Lazima wewe mkamilifu kidogo kuchukuliana na asiye mkamilifu. Usiwe hivyo mke wangu. Mvulimie ukijua siyo ndugu yako useme utamrekebisha.”
Neema alielewa kidogo maelezo hayo ya mume wake.
Kule sebuleni, Aisha naye alikuwa katika wakati mgumu sana kumwona Neema amemuita chumbani mumewe muda mfupi tu baada ya kuingia…
“Kwa nini amemuita haraka vile? Kuna nini? Au atakuwa amejua kitu kuhusu mimi na mume wake?” aliwaza Aisha.
Alikuja kutulia baada ya Neema kutoka akionesha furaha na uchangamfu.
***
Siku tatu mbele ilikuwa sikukuu, wafanyakazi hawaendi makazini. Neema, Aisha na Bony ni miongoni mwao. Lakini Nancy pia hakwenda kazini siku hiyo.
Kwenye saa tano asubuhi, Nancy alimpigia simu Neema na kumwambia anakwenda kwake amuwekee chakula…
“Wala usijali shosti, msosi upo wa kushiba na kusaza, wewe njoo tu,” alisema Neema alipoongea na simu na Nancy.

Nancy alijiandaa, akijua kuwa, nyumbani kwa Neema atamkuta na Bony, hivyo siku hiyo alivaa utatautata sana. kigauni cha kubana mwili, kifupiii mpaka basi! Kwa hiyo magoti yote yalikuwa wazi huku sehemu kubwa ya mapaja nayo ikiwa nje. Na vile alikuwa na mapaja meupe we acha tu!
Alijisiliba wanja kuliko siku aliyomsimamia ndoa Neema. Rangi ya midomo ungeweza kusema alipakia brashi ya rangi ya nyumba. Nyusi alizitinda kama vile alitumia kisu cha wachinja ng’ombe buchani.
Alichukua Bajaj hadi nyumbani kwa Neema…
“Ngo ngo ngo…wenyewe,” alibisha hodi…
“Karibu…ooo karibu sana shemeji,” Bony ndiye aliyemkaribisha Nancy, Neema na Aisha walikuwa jikoni, Neema akatoka haraka sana aliposikia sauti ya Nancy…
“Karibu shosti wangu jamani,” Neema alimkaribisha Nancy lakini alipata mshtuko kumwona shoga yake huyo amevaa kama anakwenda klabu za usiku, akajikaza kumwambia.
Baada ya salamu nyingi, Neema akampa juisi mgeni wake, lakini akaenda jikoni kumwambia Aisha kwamba aandae chakula kwani mgeni aliyemwambia kaja.

Walishirikiana kutenga chakula huku sebuleni Nancy akiteta kwa mbali na Bony…
“Vipi utatoka baadaye?” Nancy alimuuliza Bony.
“Napenda iwe hivyo?”
“Basi utaniambia tuwe wote kama hutajali,” alisema Nancy.
Wakati wanapeleka chakula kwenye meza ya chakula, Neema alikosa raha kuona jinsi mapaja ya Nancy yanavyoonekana waziwazi mpaka aibu.

Nancy na Aisha wakakutana macho, wakakumbukana. Nancy alishangaa sana kumkuta Aisha nyumbani kwa Neema wakati kule baa aliingia na Bony wakiwa wameshikana mikono…
Je, unajua nini kilitokea? Usikose kusoma kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda, Jumatatu ijayo

Leave a Comment