×

The Angel of The Darkness (Malaika wa Giza)-66

Watoto wawili mapacha, Arianna na Brianna wanatenganishwa wakiwa bado wadogo kufuatia tukio baya la kigaidi linalotokea wakiwa mapumzikoni na wazazi wao nchini Kenya, kwenye kituo kikubwa cha biashara cha Kikuyu Mall jijini Nairobi.
Katika tukio hilo, baba wa watoto hao, Joseph Ndaki, Meneja wa Benki Kuu ya Tanzania, Tawi la Dar es Salaam na mkewe, Asia Mustafa wanapigwa risasi na magaidi hao na kupoteza maisha, wakiwaacha watoto wao wakiwa bado wachanga.
Kila mmoja anapitia maisha tofauti kabisa, Arianna anarejeshwa Tanzania wakati Brianna anaokotwa na mwanamke mwendawazimu, Mashango ambaye anaishi naye kwenye mtaa wa watu maskini jijini Nairobi uitwao Mathare.
Arianna anapata bahati ya kukutana na Msuya, mfanyabiashara mkubwa ambaye anampenda kwa dhati na kuamua kumuoa. Baadaye, Arianna ananasa ujauzito wa Diego na wanapanga njama za kutoroka.
Msichana huyo anafanikiwa kutorokea nchini Kenya, jambo linalomfanya Msuya atangaze dau nono.
Hatimaye, pacha wa Arianna, Brianna anapatikana na kila mtu anaamini kwamba ndiyo Arianna na Diego anashiriki kuandaa mpango wa kumuaminisha Msuya kwamba huyo ndiye Arianna na tayari amefika nyumbani kwa Msuya lakini anaonesha tofauti kubwa ya kitabia na Arianna, jambo linalomshangaza kila mtu.
Je, nini kitafuatia? SONGA NAYO…

Hawakuelewa ‘Arianna’ amekumbwa na nini mpaka abadilike kiasi hicho kitabia na kuwa mpole, mnyenyekevu, mstaarabu na mtu anayestahili kweli kuwa mama wa familia.
Diego hakutaka kukaa sana sebuleni hapo, akatoka na kurudi chumbani kwake, Msuya akaendelea kukaa pale sebuleni na wanaye ambao walianza kumuuliza kwa nini mama yao anawaonesha mapenzi makubwa kiasi hicho.
“Jamani kwani nyie hampendi mama yenu awe mpole?”
“Tunapenda dad (baba), tunataka kila siku awe hivihivi,” walisema watoto hao, kauli iliyomfurahisha sana Msuya, moyoni akawa anamuomba Mungu wake mkewe aendelee kuwa na tabia hizohizo alizoanza kuzionesha.
Baada ya kumaliza kusafisha vyombo vilivyotumika kwa kifungua kinywa, Brianna hakuwa na muda wa kupoteza, walianza kuandaa chakula cha mchana kwa kushirikiana na wafanyakazi hao, Msuya na wanaye wakaendelea kupigwa na butwaa.
Arianna waliyekuwa wakimfahamu, hakuwa mtu wa kufanya kazi yoyote zaidi ya kuoga, kujipodoa na kujifungia chumbani mchana kutwa akibembea baada ya kujidunga madawa ya kulevya, huku mara chache alizokuwa akitoka, akifoka hovyo ndani ya nyumba hiyo. Hakuna aliyekuwa na majibu juu ya mabadiliko hayo ya ghafla ya msichana huyo.
Kwa kuwa siku iliyopita Msuya alishajiapiza kwamba ni lazima aende na mkewe hospitalini ili akampime kijanja kuona kama bado alikuwa na ujauzito wake au la, ilibidi ainuke pale alipokuwa amekaa na wanaye, akamfuata mkewe aliyekuwa akiendelea kusaidiana na wale wafanyakazi kuandaa chakula cha mchana.

“Tunahitaji kuzungumza mpenzi wangu, twende chumbani,” alisema Msuya huku akianza kupanda ngazi kuelekea chumbani kwake. Brianna aliacha kila alichokuwa anakifanya, harakaharaka akaanza kumfuata Msuya mpaka chumbani.
“Naomba uache hizo kazi unazofanya kuna mahali nataka unisindikize, kaoge ujiandae,” alisema Msuya huku akifungua kabati na kumchagulia mkewe nguo za kuvaa, na yeye akachagua zake na kuanza kumsubiri Brianna ambaye kama kawaida yake aliingia bafuni na nguo alizokuwa amezivaa pamoja na zile alizochaguliwa na mumewe.

Muda mfupi baadaye, alitoka akiwa ameshaoga na kubadilishia nguo hukohuko bafuni, Msuya akawa anacheka mwenyewe kimyakimya. Naye ilibidi aingie kuoga na dakika kadhaa baadaye, wote tayari walikuwa wameshamaliza kujiandaa.
Wakatoka mpaka kwenye maegesho ya magari ambapo tofauti na siku zote ambazo Arianna alikuwa akikaa kwenye siti ya pembeni ya dereva, alifungua mlango na kupanda nyuma. Ikabidi Msuya ashuke na kwenda kumfungulia mlango wa mbele, akashuka na kwenda kukaa siti ya mbele.

“Funga mkanda basi mke wangu, mbona leo kila kitu unafanya tofauti?” alisema Msuya kwa sauti ya masihara kwani hakutaka kumkasirisha mkewe, tabasamu likiwa limechanua kwenye uso wake. Brianna akaanza kuhangaika kufunga mkanda kwani kiukweli hakuwa akijua, ikabidi Msuya amsaidie huku akiangua kicheko.

Gari la kifahari aina ya Chevrolet la rangi ya weusi wa kung’aa, lilianza kutoka taratibu kwenye maegesho, mlinzi akafungua geti na gari hilo likaondoka kwa mwendo wa wastani, Msuya akiwa amekaa nyuma ya usukani, pembeni yake Brianna akiwa ametulia kama maji mtungini.
“Kwani tunaenda wapi?”
“Nataka tupitie hapo hospitalini kuna rafiki yangu daktari tunaenda kumuona kisha baada ya hapo tutaenda hotelini kupumzika kidogo, leo nataka tubadilishe mazingira.”
“Sasa si tungewachukua na watoto?”
“Waache wapumzike, leo ni siku maalum ya mimi na wewe,” alisema Msuya huku akiachia tabasamu pana. Japokuwa mabadiliko aliyokuwa nayo mkewe yalikuwa yakimshangaza, ukweli kutoka ndani ya moyo wake ni kwamba alikuwa akiyafurahia sana.

Breki ya kwanza ilikuwa ni hospitalini ambapo tayari Msuya alikuwa ameshampigia simu daktari wake na kumueleza juu ya mpango wake, walipofika tu alimtuma nesi kuwapokea na kuwapeleka moja kwa moja mpaka ofisini kwake.
“Mke wangu, samahani naomba daktari akupime vipimo vichache ili kujua maendeleo ya mtoto wetu tumboni,” alisema Msuya, kauli iliyomshtua sana Brianna. Alitamani kukataa lakini akahisi atamuudhi Msuya, akaamua kukubali kwa shingo upande, akaanza kupimwa huku machozi mengi yakimtoka.

“Usilie mke wangu, kwa hali yoyote itakavyokuwa, wewe bado ni mke wangu na nitaendelea kukupenda maisha yangu yote,” Msuya alimbembeleza baada ya kuona hali yake imebadilika kabisa.
Kidogo kauli hiyo ilimfariji Brianna, akajiapiza kuwa atadanganya kwamba ujauzito wake uliharibika ili kuendelea kuficha siri kubwa iliyokuwa ndani ya moyo wake.
“Mh! Daktari aliguna huku akirudia upya kutazama majibu ya kipimo cha ‘ultra sound’, akamuita pembeni Msuya na kuanza kuzungumza naye.

“Inaonesha hana mimba, hata sielewi nini kimetokea.”
“Mungu wangu, sasa kama imeharibika si itakuwa hatari zaidi?”
“Kwani mwenyewe ukimuuliza anasemaje?”
“Hasemi chochote si unajua tangu apatwe na yake matatizo, akili yake bado haijatulia kabisa. Hata hapa kupima nimefanya kumlazimisha, alikuwa hataki kabisa.”
“Ni hatari sana kama ujauzito umeharibika na hajasafishwa kizazi, kuna dawa inabidi nimuandikie akaanze kunywa leoleo, baada ya siku tatu umlete tena,” alisema daktari huyo, akarudi pale kitandani alipokuwa amelala Brianna, akampa pole na kumtaka anywe dawa atakazopewa bila kuacha hata mara moja.
“Unaweza kuharibu kizazi chako na usipate tena ujauzito, ilitakiwa useme mapema mama,” alisema daktari kwa upole, Brianna akabaki kimya kabisa kwani ukweli ni kwamba hakuwahi kukutana kimwili na mwanaume wala hakuwahi kupata ujauzito.

Baada ya hapo waliandikiwa dawa, wakatoka mpaka walipoliacha gari lao huku Msuya akionesha kuumizwa mno na taarifa zile. Zaidi akawa anamuonea huruma mkewe kwani alijua ni kwa kiasi gani anapitia kipindi kigumu.
“Ulipaswa kuniambia mke wangu ili nikusaidie,” alisema Msuya huku akilia kama mtoto mdogo, wakiwa ndani ya gari lao palepale kwenye maegesho ya hospitali.
“Nisamehe,” alisema Brianna huku akilia, kwa mara ya kwanza Brianna akakubali kukumbatiwa na Msuya kwani alionesha kuumizwa sana na kilichotokea, mwili wa msichana huyo ukawa unasisimka kuliko kawaida kwani hakuzoea kabisa mambo hayo.

“Pole mke wangu, leo inabidi tukalale hotelini, tukae wawili tu kama ilivyokuwa kwenye honeymoon yetu, si unakumbuka tulivyopata raha?” alisema Msuya huku akijidfuta machozi pamoja na kumfuta mkewe, Brianna akawa anatingisha kichwa kukubali kila kitu japokuwa ukweli ni kwamba alikuwa haelewi chochote.
Baada ya kila mmoja kutulia, waliondoka hospitali hapo na kwenda kwenye hoteli ya kifahari ya Crater View, iliyokuwa inatumiwa sana na watalii. Msuya akalipia kila kitu ikiwa ni pamoja na chakula cha mchana na usiku, wakaingia ndani ya vyumba vya kisasa vya hoteli hiyo.
Kama ilivyokuwa mara ya kwanza, Msuya alimkumbatia tena Brianna, akashindwa kumzuia zaidi ya kutulia huku mapigo ya moyo wake yakizidi kuongezeka kasi.

Je, nini kitafuatia? Usikose Jumatatu kwenye Gazeti la Ijumaa Wikienda.

1 Comment

Leave a Comment