×

Fedha za Majini Zilivyoniendesha Puta 08

ILIPOISHIA

Kumbe alimtoa mhanga mke wake na mjukuu wake. Mwenyewe amekufa na siri imefichuka!”
“Sasa naomba msaada wako.”
“Ulitaka nikusaidieje?”
“Kwanza uwaokoe mama yangu na mwanangu ambao wanateseka kule pangoni. Na pili ninataka kuepukana na zile pesa. Mimi sizitaki tena.”
Mganga akacheka.
“Kwa nini huzitaki?”
“Masharti yake ni magumu kwangu. Yule jini aliniambia niende nikamzini makaburini. Sitaweza.”
“Lakini baba yako aliyaweza yote hayo.”
“Kosa alilofanya ni kunifanya mimi kuwa mrithi wake wa pesa zile na kwa hivyo ninatakiwa nimrithi na yule jini wake jambo ambalo sitaliweza. Baya zaidi ni kuwa ninatakiwa nimtoe kafara mke wangu ili mama yangu akifa pawepo na mtu mwingine.”

SASA ENDELEA

Kwa kweli ni tatizo. Lakini kuna watu wengine wanazitaka hizo pesa za majini na wako tayari kuwatoa kafara ndugu zao au wazazi wao pamoja na watoto wao.”

“Ni kweli watu hao wapo na mmojawapo ni huyo marehemu baba yangu. Hakujali kumtoa kafara mke wake na mjukuu wake ili apate pesa.”
“Nikwambie ukweli kuwakomboa mama yako na mwanano litakuwa ni tatizo kwa sababu yule jini anayehusika hivi sasa unaye wewe.”
Aliponiambia hivyo nilishituka.
“Mimi siko naye,” nikamwambia na kuongeza.
“Sijakubaliana naye.”
“Makubaliano ni yale ya jini huyo na baba yako kwamba atakapokufa yeye mrithi utakuwa ni wewe. Kwa hiyo baada ya baba yako kufa, wewe ndiyo umemrithi huyo jini!”
Nikajishika kichwa na kukitikisa kusikitika.
“Huu ni upuuzi. Ushirikina wao utanihusu nini mimi? Huyu baba alikuwa mtu wa aina gani!” nikajisemea kisha nikamuuliza yule mganga.
“Yaani haitawezekana kuwakomboa mama yangu na mwanangu?”
“Haitawezekana.”
“Haitawezekana hata kama sizitaki zile pesa zao, wachukue wenyewe?”
Niliporudia kutaja pesa yule mganga alitulia kimya. Nikamuona kama alikuwa akiwaza kitu.
“Una uhakika kwamba hizo pesa huzihitaji?” akaniuliza baada ya ukimya mfupi.
“Sizihitaji. Namuhitaji mama yangu na mwanangu!” nilimwambia kwa sauti kali ili aweze kunielewa vizuri..
“Na una uhakika kwamba hujazitumia hata kidogo?”
“Sijazitumia na sitazitumia.”
“Sasa sikiliza, niletee mimi hizo pesa kama huzihitaji. Mimi nitajua jinsi ya kuzifanya.”
“Lakini nakuomba uzingatie tatizo la msingi!”
“Tatizo la msingi ni lipi?’
“Ni kuwapata mama yangu na mwanangu.”
“Mama yako na mwanano utawapata kwa sababu hizo pesa utakuwa umezitoa kwa mtu mwingine. Mimi ndiye nitakaye beba jukumu hilo.”
“Na lile jini litakuja kwako?”
“Hilo jini linakuwa na mtu anayemiliki hizo pesa. Kama wewe umezitoa halitakaa kwako tena.”
“Mimi nitakuwa huru?”
“Ndiyo. Wewe utakuwa huru.”
“Sawa. Sasa hizo pesa ziko kwenye sanduku la chuma. Kulileta kwako muda huu haitawezekana lakini kama tutasaidiana kulibeba wakati wa usiku, tunaweza kulileta hapa kwako.”
“Una maana kwamba limejaa pesa hadi juu?”
“Limejaa mpaka pomoni na ni nyekundu tupu!”
Mganga alitoa ulimi akaupitisha kwenye mdomo wake wa juu kwa tamaa. Akaniambia.
“Tufuatane sasa hivi hadi nyumbani kwako, niende nikaziangalie.”
“Twende.”
Hapo hapo mganga akainuka.

“Nisubiri kidogo.”
Aliingia kwenye chumba kimojawapo. Baada ya muda kidogo akatoka akiwa amevaa suruali na shati jingine.
“Twenzetu,” akaniambia.
Tukatoka. Mganga hakutaka tupande bodaboda, alitaka twende kwa miguu. Tukaenda kwa miguu hadi kijijini kwetu.
Tulifika nyumbani kwangu, nikafungua mlango na kumkaribisha ndani. Nilimuingiza katika chumba changu, nikamwambia akae kwenye kiti.
Nikainama kwenye mvungu wa kitanda na kulivuta lile sanduku la chuma. Nikaona amelikodolea macho. Nilichukua funguo nikafungua ile kufuli.

Nilipolifungua lile sanduku, mganga alishituka alipoziona zile noti.
“Pesa ni tamu lakini pesa hizi zina matatizo, zitakusumbua. Zitakusababishia umkose mke wako na mama yako pamoja na mwanao,” akaniambia kwa namna ya kunishawishi nimpe yeye.
“Mimi sizitaki.”
Mganga akaendelea kuzitazama pesa hizo huku macho yake yakimeta.
“Sasa nikwambie kitu,” akaniambia.

“Niambie.”
“Mimi naona nilichukue sasa hivi hili sanduku.”
“Hutaliweza, ni zito.”
“Hebu ngoja nilijaribu.”
Mganga akajaribu kuliinua.
“Mbona ni jepesi sana. Haliwezi kunishinda. Nataka nikuondolee hili balaa. Hili ni balaa bwana!”
“Sawa. Lifunge ulichukue.”
Mganga akalifunga sanduku hilo lililokuwa wazi. Kisha akalibeba na kuliweka begani.
Itaendelea wiki ijayo

Leave a Comment