×

chongo -32

Ilipoishia wiki iliyopita
Saa mbili za usiku, Mwani na Jully walitoka, wote wakiwa wamevaa kaptura za jinzi na fulana zinazobana, nyeusi, wakazunguka nyumba mbili tatu, wakatokezea nyuma, sehemu ilipo chemba inayotokezea nyumba wanayoishi akina Jerry na mkewe!
Sasa endelea
Taa zilikuwa zinaonekana kwa mbali, mtu yeyote angeweza kuwaona, lakini siyo kuwatambua. Hata hivyo, kwa wakati huo hakukuwa na mtu aliyekuwa na taimu nao, kila mmoja alikuwa bize katika mambo yake. Jully alimtaka Mwani kufunua mfuniko wa chemba na atangulie kuingia wakati yeye anaangalia usalama.
“No, nimebadili mawazo Jully, wewe usije, ubaki hapa kwa ajili ya ulinzi, chochote kinaweza kutokea au unasemaje?” Mwani alimuuliza mwenzake.

“Hamna kitu kitakachotokea wewe, mbona tena unaanza mchecheto? Lakini kama unaona hivyo poa, nitabaki hapa, lakini nikiwa ndani ya chemba, asionekane mtu hapa juu,” Jully naye alimwambia.
Wakakubaliana, taratibu Mwani akashika mfuniko wa chemba, udongo ulikuwa mzito, lakini akafanikiwa kuufunua. Kwa kutumia mwanga wa simu yake, akamulika ndani na kuona kukiwa safi, akaingia. Shimo lilimfikia usawa wa kifua chake. Wakati wote macho ya wasichana hao yalikuwa yakiangaza huku na kule kuona kama kuna mtu aliyewafuatilia.

Mwani akainama, akaanza safari yake, ingemchukua kama dakika mbili kutambaa ndani ya chemba ile hadi kufika anapokwenda. Sekunde kumi baada ya Mwani kuondoka, Jully naye akaingia taratibu, kwa mbali akauona mwanga wa simu ya Mwani ukiyoyoma, akajikuta akipata raha. Kwa mara ya kwanza, roho ya ujasiri ikamuingia, akajiapiza kushiriki zoezi lile hadi mwisho.
Dakika ya kwanza ikapotea, ya pili, ya tatu, ya nne na ya tano…hakukuwa na dalili za Mwani kuonekana akirejea. Jully akaanza kupata wasiwasi, akainuka na kutazama juu pande zote, hakukuwa na chochote cha kutia mashaka, akarudi tena chini. Kwa mbali akaona mwanga wa simu, akafarijika!
***
Sule alikuwa amefika mtaa wa Samora mapema saa tano asubuhi, hakutaka kusimama pale nje ya jengo la Mox Mall, akawa anatembea akipandisha juu hadi mnara wa saa, tena akiteremka hadi sanamu ya askari, macho yake yakiwa bize kwa vijana waliokuwa wakiuza nguo na viatu. Sura ya Bata, yule kijana anayependa kuvaa miwani ya jua, ilikuwa kichwani mwake.

Hadi ilipofika saa tisa alasiri bila kuona chochote, akatoa simu yake na kumpigia Twaha ambaye baada ya kusalimiana na kupeana michapo miwili mitatu ya tangu walipoachana jana yake, akaomba kama wanaweza kukutana muda ule, popote pale.
Wakakubaliana wakutane eneo ambalo walipata kinywaji jana yake na saa moja na nusu baadaye, jamaa hao walikuwa pamoja katika pub moja nyuma ya Hospitali ya Palestina, ambayo pia ilikuwa na nyama maarufu ya Mbuzi Katoliki.
“Sikiliza Twaha, nahitaji demu, nile naye mtungi hafu nikalale naye,” Sule alisema mara tu baada ya kukaa na kila mmoja kuagiza kinywaji chake.

“Mbona mapema sana mzee, una tatizo kwani?” aliuliza Twaha, huku akimalizia kumimina bia yake kwenye glasi, akitingisha kichwa kumuashiria mhudumu amuongezee kinywaji. Mikono yake pia ilikuwa kwenye simu yake, ikibonyeza kitufe kimoja baada ya kingine.
Halafu akaiweka simu yake sikioni na sekunde chache baadaye, alikuwa akiongea na mtu, mwanamke. Walionekana kama watu wanaofahamiana, maana walianza kwa kutaniana kabla ya kukata simu.
“Kuna chuma kinakuja, itabidi ukigharamikie sana, maana nina orodha ya hawa wadada wanaojiuza kiofisa, dau lake linaanzia fifte kwa fasta,” Twaha alisema huku akitabasamu, kitendo kilichopokelewa kwa tabasamu kubwa pia kutoka kwa Sule.
“Sasa anakuja mmoja tu itakuwaje, wewe utakuwa unanikodolea tu mimi macho?” Sule alimuuliza mwenzake.
“Hapana kaka, mimi nina mke na nikihitaji sana kuchepuka, basi nina kadenti kangu nakashtua, hawa jamaa mimi siwawezi kabisa,” Twaha akajibu.
***
Mwanga wa simu kutoka upande ule uliokuwa amekwenda Mwani ulizidi kusogea kimyakimya na Jully akatoka kabisa nje ya chemba ili kuhakikisha usalama. Hakukuwa na mtu wa kumtilia mashaka, akachungulia tena na kumtaka Mwani atoke nje.
Mwani alitoka nje, mkono wake mmoja ukiwa umeshikilia sehemu ya katikati ya paji lake la uso kitambaa chake cha mkononi kimeloa damu!
Je, nini kilitokea? Usikose kufuatilia simulizi hii ya kusisimua katika toleo lijalo

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

SUBSCRIBE YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

Leave a Comment