×

Ndoa na Shetani- 31

ILIPOISHIA:
Baada ya zoezi lile kukamilika nilirudi nyumbani na kuanza zoezi lingine la kufumua nywele na kuziacha timutimu kisha ziliwekewa vumbi la mbao na udongo kupakwa masizi usoni na kupatiwa ndala mbovu kulwa na doto ambazo  tulizipata maeneo tuliyokuwa tunakaa zilikuwa za msalani.
Nilipigwa picha huku nikitengenezwa na mtaalam wa kutengeneza sura, akirekebisha sehemu zilizoonekana zina mushikeri.
SASA ENDELEA…
Baada ya marekebisho nilisimama na kupigwa picha zingine ambazo zilionesha nafanana na mwenda wazimu wa kweli.
Watu wale walikuwa wamejipanga kweli, pia alikuwepo mtaalam wa sanaa za jukwaani ambaye alinielekeza baadhi ya tabia za mwenda wazimu  japokuwa kwangu niliona hakuwa na msaada mkubwa sana.

Lakini sikumbishia, nilimsikiliza na kuniongezea baadhi ya vitu ambavyo niliamini vitanisaidia.
Wiki moja ilikatika huku kila mmoja akiuamini uwezo wangu, siku iliyofuata ndiyo niliyotakiwa kuanza kazi rasmi ambayo kutokana na maelezo ya Papaa ile ilikuwa njia ya kuufikia utajiri.

Moyoni nilipanga kufanya kitu ambacho hawakukitegemea kukiona kwa vile maisha yangu tangu nilipo hasi zizini yalijaa usanii. Jumatatu niliamshwa saa tisa usiku na kuandaliwa kwa mwili kupakwa rangi ya masizi  kuonesha uchafu na nywele kuwekewa vumbi la mbao na udongo kidogo kisha kuvishwa matambala machafu.
Niliposimama mbele ya kioo Konso nilijishangaa nilikuwa mwendawazimu kamili. Nilibebwa ndani ya Noah nyeusi na kwenda kuachwa karibu na soko nikiwa na watu zaidi ya wanne ambao waliangalia usalama wangu.
Niliteremka na kutembea kuelekea sokoni ambako nilijua nitakaa wapi kwa muda ule mpaka papambazuke. Mbona nilikoma kibaridi cha Nairobi, we acha tu kiliingia mpaka kwenye mfupa.

Kuna kipindi niliona kama damu inataka kusimama, nilikunywa kichupa kidogo cha pombe kali kilichonisaidia kuutia mwili joto. Najua utajiuliza hiyo pombe kali niliitoa wapi, ile nilipewa na kutakiwa kuinywa kabla hakujapambazuka ili kupunguza baridi. Kisha nilitakiwa kukomaa mpaka nitakapopata chakula.
Najua unataka kujua napataje chakula na nani anayeniletea na nikiletewa nitakulaje. Naomba twende pamoja msomaji wangu ili nisikuache hata hatua moja. Kila kitu kiliratibiwa kisayansi bila mtu kujua nini kilichokuwa kikiendelea.
Baada ya kupambazuka nilizunguka sokoni na sehemu ya jalalani, kutokana na ubize wa watu wa Nairobi walinishangaa wachache wengine walinipuuza japo wapo walinionea huruma mwanamke kama mimi kuwa mwendawazimu wapo waliosema huenda nimerogwa kwa kutembea na mume wa mtu, kila mtu alisema lake.

Muda wa kula ulipofika nilijua chakula kimewekwa sehemu gani kama jalalani kiliwekwa sehemu gani ndani ya mfuko. Kila hatua kulikuwa na mtu akisimamia zoezi. Nilifuata maelezekezo kwa kuchukua na kusogea pembeni ya jalala na kula  kisha nilipumzika  kidogo na kuendelea na safari.
Niliendelea na mizunguko yangu huku nikiwa nimeshikilia fimbo mkononi, nikitakiwa kufika maeneo mengi kwa ajili ya kujitangaza kwa watu wengi hata siku nikiponywa kimagumashi watu waamini kweli nilikuwa mwendawazimu kweli si wa kutengeneza.

Nilishika bakora na kuwatishia watu kama nawapiga lakini sikumpiga mtu zaidi ya kuwatisha na kuishia kucheka wanaponikimbia mpaka nakaa chini. Kiza kilipoingia nilifuatwa na gari kwa kwenda sehemu ya kiza na kupanda kurudishwa nyumbani.

Nilipofika nyumbani kila mtu alinisifu kwa kazi nzuri niliyoifanya. Kwa vile ilikuwa siku yangu ya kwanza nilichoka sana kutokana na kuzurura na kutopata muda wa kupumzika kama nilivyokuwa nimezoea, mchana nalala usiku kazini kama popo.

Kutokana na uchovu nilioga bila kuchana nywele kwa vile bado kazi ilikuwa inaendelea na siku ile ndiyo kwanza ilikuwa inaanza. Nilikula na kwenda kupumzika kipindi kile sikuwa karibu na Papaa kutokana na zoezi lile, hivyo nilikwenda chumbani kwangu nilikunywa pombe kidogo na kulala.
Nakumbuka siku moja baada ya kuchukua chakula changu na kusogea pembeni ya jalala chini ya mti wakati nakula, alitokea chizi mmoja wa kiume aliyenipora chakula. Kabla ya kunipora alinitandika makofi mawili mazito yaliyonifanya nione kizunguzungu.
Usikose mwendelezo wake katika gazeti la risasi jumamosi.

HADITHI ZA KUSISIMUA NA MBINU ZA UJASIRIAMALI, INGIA NA LIKE PAGE YA FACEBOOK YA ERIC SHIGONGO===>https://www.facebook.com/shigongotz/

KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA TUFOLLOW

INSTAGRAM===>https://www.instagram.com/globalpublishers/

TWITTER===>https://twitter.com/GlobalHabari

FACEBOOK===>https://www.facebook.com/GlobalPublishers

SUBSCRIBE YOU TUBE===>https://www.youtube.com/user/uwazi1

Leave a Comment