BAADA ya kukaa Hospitali ya New York Obstetrics & Gynaecology kwa siku kadhaa, Catarina amepata nafuu kubwa, hapo ndipo anaamua kufuatilia ukweli juu ya Kevin, anatafuta namba ya FBI ambao anawasiliana nao na kuwaeleza kwamba alikuwa hai, si kweli kama alikufa kama dunia inavyofahamu, jambo linalowashangaza sana FBI.
Anakwenda mbele zaidi akiwaeleza juu ya Kevin na kuomba kupata msaada wa kufahamu mahali alipo kwani alifanikiwa kumwona kwenye televisheni, FBI wanampatia namba ya mzee Thomas Edmund na kumweleza kwamba huyo ndiye angeweza kumweleza ukweli wa mahali alipo Kevin. Anashukuru, kuagana nao kisha kukata simu.
Upande wa pili wazazi wa Catarina na Kevin nao pia wanafanikiwa kumwona Kevin katika televisheni na kuamua kufuatilia na kugundua hoteli aliyokuwa amefikia, wanafika hapo na kujitambulisha na kitambo kifupi tu wanafanikiwa kukutana na Kevin ambaye anawasimulia kila kitu kilichomtokea na jinsi mtu aliyeitwa Jamal alivyotaka kumuua ndani ya hifadhi ya American.
Muda mfupi wakiwa hapo simu ya mzee Thomas inaita na anapoipokea mtu upande wa pili anajitambulisha kama Catarina akiwa katika Hospitali ya New York Obstetrics & Gynaecology jambo linalowashangaza wote. Kwa pamoja wanaelekea huko na kufanikiwa kuonana naye, wanakumbatiana kwa furaha, hapo ndipo mama Catarina anaomba waombe kwanza kumshukuru Mungu na mengine yote yangefuata. Wanapiga magoti na kufumba macho, lakini ghafla mlango wa chumba unafunguliwa na Jamal anaingia. Je, nini kitaendelea?
SONGA NAYO…
“
Baba nakushukuru kwa muujiza huu, hakika hii ni kazi yako, malaika wako walikuwepo kuwalinda watoto wetu, pamoja na kupita kwenye milima na mabonde mengi, lakini mwisho wa siku umetukutanisha watoto wetu wakiwa hai najua umefanya jambo hili litokee kwa kusudi uliloliandika wewe Mungu lazima litimie! Pengine ni watoto ambao kama Catarina na Kevin wangekufa wasingezaliwa, nakuomba Mungu ukatimize kile ambacho wewe umekipanga, kila kitakachotokea mapenzi yako yatimizwe…” mama yake Catarina alimaliza kusali machozi yakimbubujika.
Karibu kila mtu ndani ya chumba alikuwa akilia, Catarina akiwa hajiwezi kabisa na vivyo hivyo Kevin, hawakufahamu ni nani aliyeingia chumbani wakiwa katikati ya sala, akilini mwa baadhi yao walidhani pengine alikuwa ni muuguzi au daktari, waliendelea kufumba macho mama yake Catarina akisali, ilikuwa ni sala ndefu iliyojaa hisia.
Jamal alikuwa kimya akisikiliza kwa makini sala hiyo ambayo ilimwonyesha kwamba mtu aliyempeleka porini ili afe kwa kuliwa na wanyama wakali na hatimaye yeye kubaki na Catarina, alikuwa ndani ya chumba hicho.
Hofu mbili kuu zikamwingia; ya kipigo na ya kunyang’anywa mke, zilimfanya ashindwe kuyazuia machozi yake pia! Mashavu na shingo yake vikalowa. Alimpenda Catarina kupita kiasi, kwake hakuwa mwanamke tu bali mfariji wa maisha yake na hakuwa tayari kuachia awe mke wa mwanaume mwingine chini ya jua la Mungu.
“I will fight for my right, Catarina loves me, there is no way she can leave me for another guy!”(Nitapigania haki yangu, Catarina ananipenda, hakuna namna anaweza kuniacha mimi na kwenda kwa mwanaume mwingine!) aliwaza akijipa moyo hasa alipofikiria jinsi alivyookoa maisha yake.
“Ninaomba hayo yote katika Jina la Baba, Mwana na Roho Mtakatifu….”
“Amen!” watu wote ndani ya chumba wakaitikia na kufumbua macho yao.
***
Kulikuwa ni kuchanganyikiwa kwa hali ya juu sana kwa Jamal, kilichotokea kilikuwa ni kitu ambacho hakuwahi kukiwazia kwa jinsi yeye na Catarina walivyoishi akiwa amesamehewa tukio la kumuua Kevin msituni! Atoroke? Kwenda kwa Kevin? Haiwezekani, alijiuliza maswali na kujijibu mwenyewe.
Kwa siku mbili akiwa haamini kama Catarina kweli alitoroka kwenda New York aliendelea kumtafuta hapohapo mbugani na miji ya jirani bila mafanikio, mwisho akaelewa kilichotokea ulikuwa ni mpango wa mauaji, uliopangwa vizuri ili kufanya ionekane kama Catarina ametoroka kwenda kuungana na Kevin, jambo ambalo Motown na kundi lake lililobaki walikuwa na uwezo wa kulitenda, hata hivyo Jamal aliamua kusafiri kwenda huko New York kufuatilia.
Akiwa ndani ya treni alianza upelelezi wake kwa kuzungumza na wafanyakazi, wa kwanza tu aliyeongea naye, alitambua tukio la kusafiri na mwanamke mjamzito aliyekuwa akiumwa tumbo na kuvuja damu! Alipodadisi kuhusu muonekano wake aliambiwa mwanamke huyo alikuwa ni Mwafrika, akawa na uhakika kabisa alikuwa ni Catarina.
“Mlipofika New York, nini kilitokea?”
“Gari la wagonjwa lilikuja, akapakiwa, mimi nilikuwa miongoni mwa watu waliomsindikiza mpaka hospitalini!”
“Hospitali gani?”
“New York Obstetrics & Gynaecology”
“Ahsante sana!”
“Mbona umeulizia sana?”
“Ni mfanyakazi mwenzangu.”
“Sijui kama amepata nafuu, maana damu nyingi sana zilikuwa zikimtoka.”
“Alikuwa na fahamu?”
“Hapana.”
“Ahsante.”
Jamal akiwa amechanganyikiwa, maelezo ya kijana huyo yalizidi kumvuruga, hata hivyo akaweza kusafiri mpaka New York ambako alishuka na kuitafuta hospitali ya New York Obstetrics & Gynaecology mpaka akaipata, moja kwa moja akaelekea kwenye idara ya kumbukumbu za wagonjwa na kuulizia kama walimfahamu Catarina.
“Ndiyo!”
“Amelazwa wodi gani?”
“Ya wagonjwa mahututi wanawake!”
“Iko upande gani?”
“Nyoosha kupitia hapa, pale mbele kata kulia, utaliona jengo kubwa limeandikwa ICU, bonyeza kengele!”
Hicho ndicho alichokifanya baada ya kufikia jengo hilo, akatokeza muuguzi aliyevalia nguo za kijani na viatu vikubwa vya plastiki vyenye rangi nyeupe na kumuuliza kama alikuwa na shida yoyote, Jamal akataja jina la Catarina na kuulizia kama alikuwa ndani ya wodi hiyo.
“Hapana, hapa ametolewa leo, yuko wodi ile paleee ya wagonjwa wa kawaida!” muuguzi alimwambia Jamal akiisonta wodi hiyo.
“Nashukuru sana!”
Jamal alitembea hadi kwenye wodi hiyo, nako pia akakutana na muuguzi na kumuuliza chumba alicholazwa Catarina, akaonyeshwa, moyo ukimdunda na jasho jingi kumtoka, lakini akiwa na furaha kwamba Catarina alikuwa hai, aliusogelea mlango na kugonga, hakuna mtu aliyefungua ndipo akaamua kuingia hadi ndani na kuwakuta watu wamepiga magoti wakisali, Catarina akiwa miongoni mwao, yeye pekee ndiye aliyemfahamu.
***
Watu wote ndani ya chumba hicho walifumbua macho yao na kuanza kuangaliana, macho ya Kevin yakatua kwa Jamal ambaye macho yake yote yalikuwa yameelekezwa kwa Catarina, akimsogelea ili amkumbatie! Hasira ikampanda Kevin, hasa alipokumbuka kitendo ambacho Jamal alimfanyia porini ili aliwe na wanyama wakali.
“What are you doing here you bastard? Have you forgotten what you did to me? God has brought you before me for fierce punishment!” (Unafanya nini hapa Mwanaharamu wewe? Umesahau mambo uliyonitendea? Mungu amekuleta mbele yangu ili upate adhabu kali!) Kevin aliongea kwa sauti ya juu watu wote ndani ya chumba wakimshangaa, mkononi alikuwa ameshikilia kisu chenye ncha kali tayari kwa kumchoma Jamal.
Je, nini kitaendelea? Nini hatima ya penzi la Jamal na Catarina? Fuatilia siku ya Ijumaa katika Gazeti la Championi Ijumaa.