Na Stephano Mango, RISASI Mchanganyiko
RUVUMA: JESHI la Polisi Mkoani Ruvuma linawashikilia waendesha bodaboda 20 wa Manispaa ya Songea kwa tuhuma za kumshambulia na kumjeruhi askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ) wa kikosi cha 411 KJ cha Ruhuwiko kilichopo mjini hapa baada ya kumgonga mtembea kwa miguu.
Tukio hilo lilitokea hivi karibuni baada ya askari huyo, Samuel Nginila akiwa anaendesha gari lenye namba za usajili, T 967 DAE, aina ya Nissan Xtrail kudaiwa kumgonga Bahati Mbero katika eneo la Majengo mjini hapa baada ya kutokea ghafla barabarani.
Baada ya kumgonga, inadaiwa madereva wa bodaboda walimzingira na kutaka kumpiga, lakini katika kujihami, askari huyo aliendesha gari kuwakimbia, lakini alipofika eneo la Mfaranyaki, tairi la gari hilo lilichomoka na hivyo kukutwa na waendesha bodaboda hao waliomshushia kipigo sambamba na kulichoma moto gari lake.
Licha ya kumjeruhi askari huyo, watu wengine waliokuwa wamepanda gari hilo pia walijeruhiwa, ambao walitajwa kuwa ni Kaumbya Kateka (24) mkazi wa Majengo, Joyce Edson (24) mkazi wa Mpambalyoto na Jackline Mwita (22), mwanafunzi wa Chuo cha Uuguzi Peramiho.
Kamanda wa Polisi mkoani Ruvuma, Zuberi Mwombeji alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema msako wa kuwakamata watu zaidi waliohusika katika tukio hilo, lililosababisha upotevu wa baadhi ya vitu vya askari huyo, zikiwemo pesa taslimu shilingi 120,000 unaendelea.