ILIPOISHIA WIKI ILIYOPITA
Bilionea Elizabeth anapendwa na mpenzi wake, James, bila mtoto, mapenzi yanaonekana si mapenzi, hataki kitu kingine zaidi, kila siku kazi yake ni kumwambia Mungu kwamba anataka mtoto tu. Je, nini kiliendelea?
SONGA NAYO…
Hakukuwa na kipindi kigumu kilichowahi kutokea katika maisha yake kama hicho, kila alipopita, alihisi watu wakimnyooshea vidole na kumwambia kuhusu suala la kupata mtoto, akakesha akilia, alikosa amani kabisa katika maisha yake.
James hakumuacha, alikuwa akimfariji kila siku kwa kumwambia kwamba suala la kuwa na mtoto, Mungu ndiye aliyeamua nani awe naye na nani asiwe naye. Japokuwa maneno hayo yalimfariji lakini bado aliendelea kulia mno.
Alimuomba sana Mungu tena kwa kutoa sadaka, maadui zake waliendelea kumsema vibaya huku maneno yakiongezeka na kuitwa malaya na watu wengi waliokuwa wakimchukia huku wengine wakianza kuweka picha kwenye mitandao wakiwa na watoto wao na kuandika maneno yaliyoonekana kama dongo kwake.
“Mchungaji naomba uniombee….” alimwambia Mchungaji Kimaro wa Kanisa la Praise And Worship.
“Unahitaji nini Elizabeth?”
“Nahitaji kuwa na mtoto.”
“Hilo tu?”
“Ndiyo!”
“Usijali! Mungu anatenda mambo yake kwa wakati, ila inakupasa uolewe kwanza,” alisema mchungaji huyo.
“Nitapata mtoto kweli?”
“Mwamini Mungu! Utapata tu. Hakuna linalomshinda aliye juu,” alisema mchungaji huyo.
Kidogo maneno hayo yakamfariji kwa kuona inawezekana kwamba Mungu alitaka aanze kupata mtoto akiwa ndani ya ndoa, alichokifanya ni kuzungumza na James na kumwambia dhamira yake kubwa ya kutaka kuolewa naye.
Alijua kwamba msichana huyo hakuwa na uwezo wa kupata mtoto lakini hilo hakutaka kujali, kila kitu alichokiona ni kuhusu moyo wake. Sababu haikuwa fedha, sababu haikuwa maisha mazuri, alichokifikiria kwa wakati huo ni mapenzi mazito aliyokuwanayo kwa msichana huyo.
Alimpenda sana Elizabeth, hakukuwa na mwanamke aliyekuwa na thamani kubwa moyoni mwake kama aliyokuwanayo msichana huyo, suala la kumuoa, wala halikuwa tatizo kwake, akakubaliana naye kwani pia alipofikiria kuhusu wema aliomfanyia, alijisikia kuwa na deni kwa msichana huyo.
“Umekubali?’ aliuliza Elizabeth.
“Nimekubali mpenzi,” alijibu James.
Alichokifanya ni kuwaambia marafiki zake wa karibu kwamba alitarajiwa kuolewa hivi karibuni hivyo alimkaribisha kila mtu kuhudhuria harusi hiyo ya kipekee. Watu hawakuamini, walimfahamu sana Elizabeth, ilikuwaje akubali kuolewa kirahisi namna hiyo na wakati wanaume wengi walijaribu kufanya hivyo ila alikataa.
“Mbona umeamua ghafla?” aliuliza
“Basi tu! Nimeamua nifunge ndoa, si unajua nishakua mtu mzima sasa!” alisema Elizabeth.
Taarifa za harusi hiyo zikaanza kuandikwa sehemu mbalimbali, watu wengi wakatamani kuifuatilia harusi hiyo iliyowafanya watu maarufu kutoka nchi nyingine kwenda nchini Tanzania kwa ajili ya kushuhudia tu.
Tetesi zikaanza kusikika kwamba harusi hiyo ilitarajiwa kufanyika ndani ya ndege, wengine wakasema kanisani lakini kuna watu wengine walisema kwamba harusi hiyo ilitarajiwa kufanyika katika moja ya boti kubwa na ya kifahari ambayo iliagizwa kutoka nchini Italia, kila mtu alisema lake.
Elizabeth hakutaka kuzungumzia juu ya mahali ambapo harusi hiyo ingefanyika, alichokitaka ni watu kusubiri na kuona kwa macho yao. Shela la bibi harusi likaagizwa kutoka nchini Ufaransa huku suti ikiagizwa kutoka nchini Uholanzi, kwa kifupi maandalizi yalikuwa yakiendelea vizuri.
Kila kitu kilichokuwa kikiendelea James hakuamini kabisa, hakuamini kama kweli alikuwa akienda kuwa mume wa Elizabeth, msichana maarufu na bilionea barani Afrika. Taarifa zile zilisambazwa kama upepo, japokuwa kilikuwa kimebaki kipindi cha mwezi mmoja lakini kila mtu akawa na hamu ya kushuhudia harusi hiyo ambayo ilionekana kama kulazimishwa na msichana Elizabeth.
Kila mmoja alitaka kushuhudia harusi iliyokuwa ikizungumziwa kila kona, wengine walisema kwamba ingevunja rekodi nchini Tanzania na kujitengenezea historia yake.
Kuolewa kwa Elizabeth halikuwa jambo la kukaa kimya, utajiri na umaarufu wake uliendelea kutikisa barani Afrika kiasi kwamba chochote kile ambacho ungefanya, basi ilikuwa ni lazima kumzungumzia yeye.
Hapo ndipo watu wenye akili zao, watu waliozaliwa kwa ajili ya kutafuta fedha duniani wakaanza kufanya kile walichoamini kwamba kingewaingizia fedha. Jarida la Teenegers lililokuwa likitoka kila mwezi nchini Tanzania likatoa kopi za haraka zaidi ya elfu sabini ambapo mbele kabisa kulikuwa na picha kubwa iliyomuonesha Elizabeth akiwa na James tena huku wakiwa kwenye mavazi ya harusi, kila aliyeliona jarida lile, aliingiza mkono mfukoni, akatoa fedha na kulinunua.
Nini kiliendelea? Fuatilia wiki ijayo.
SOCIAL MEDIA ZETU:
KWA HABARI ZA KITAIFA, KIMATAIFA, MASTAA NA MIKASA YA KUSISIMUA
INSTAGRAM: @Globalpublishers
TWITTER: @GlobalHabari
FACEBOOK: @GlobalPublishers
SUBSCRIBE YOU TUBE: GlobalPublishers
GLOBAL TV ONLINE: www.globaltvtz.com