×

Ishu siyo kusaidia tu bali unamsaidia nani na kwa nini?

Maisha ni fumbo kubwa ambalo hakuna ajuaye nini kitatokea sekunde mbili zijazo! Kila wakati huwa tuko katika fumbo hili. Ndiyo maana karibu kila kitu kitokeacho duniani huendelea kuwa kipya kwa sababu hakuna awezaye kujua nini kinaweza kutokea muda mchache ujao.

Kutokana na hilo ndiyo maana leo nataka kukupa elimu juu ya kuwa na moyo wa kuwasaidia wale wanaostahili kusaidiwa. Kwa kufanya hivyo, utakuwa unajiwekea kumbukumbu bora na njema sana hata pale ambapo utakuwa haupo.
Hakuna uwekezaji mzuri katika maisha kama kuwekeza kwa watu na kumbuka hakuna aliyewahi kufilisika kwa kusaidia watu.

Huu ndiyo ukweli kuhusu maisha. Jukumu la kuishi maisha ya kusaidia ni letu sote. Ukisaidia leo, hakika kuna siku ambayo msaada wako utakurudia katika hali ambayo hukuitarajia.

Hii ni kwa sababu wakati wa kutoa, huwezi kujua Mungu atakurejeshea kwa njia gani. Muhimu ni wewe kusaidia.
Sisemi kuwa uwe ni mtu wa kutoa na kuachia pesa na vitu vyako ovyo. Hapa nazungumzia kusaidia walio na uhitaji wa kusaidiwa. Kitendo cha kwenda baa na kusaidia walevi wanaoomba mia tano ya viroba, huo siyo msaada bali ni ufujaji wa pesa!
Epuka kusaidia watu ambao kwa hakika wana nguvu na uwezo mkubwa wa kufanya na kutenda mambo. Unakuta mtu ana nguvu na uwezo mkubwa kiakili, lakini badala ya kufanya kazi kwa nguvu na kujitegemea, anakuwa ni mtu wa kuombaomba. Hakuna umuhimu na ulazima wa kumsaidia mtu wa namna hiyo.

Rai yangu katika makala haya ni wewe kumsaidia mtu ambaye hata kwa kumuangalia tu anaonekana kweli anahitaji msaada.

Tuwe makini sana na watu wanaoomba msaada. Wengi wao hujivisha hali ya umaskini na uso wa kutia huruma, lakini baada ya kupokea msaada wanaouhitaji, hukimbilia kwa ‘mama muuza ulabu’ na kujimiminia glasi za pombe za kienyeji.
Ndiyo maana nikasema, kuwa makini sana na watu wanaoomba msaada kwako. Lakini ukishajiridhisha kuwa mtu anayekuomba ana uhitaji, kama una uwezo kumsaidia ni jukumu lako na hapo hupaswi kuwa na maswali ya kujiuliza. Angalizo langu ni kuwa makini na watu wanaoomba msaada.

Ndugu zangu, unaweza usione faida na umuhimu wa kusaidia kwa sasa, lakini napenda kukusisitiza wewe msomaji wangu kwamba, kuna faida kubwa sana kusaidia maishani. Endelea kutoa na Mungu atakuzidishia.
Kadiri unavyotoa, ndivyo Mungu anazidi kukubariki na kukuongezea kipato chako. Ishi vyema na watu. Waone kama ni ndugu na sehemu ya maisha yako. Wapende kama unavyojipenda.

Leave a Comment