×

Naibu Waziri Mavunde: Nilivyomkamata Mmachinga wa Kichina

MAVUNDE

Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu; Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu, Anthony Peter Mavunde mwishoni mwa wiki iliyopita alifanya mahojiano na Wahariri Wetu, Elvan Stambuli na Sifael Paul katika Hoteli ya Atriums jijini Dar es Salaam akazungumzia mengi kuhusu ajira, vijana na walemavu. Ungana nasi katika makala haya sehemu ya kwanza:

Serikali ina mikakati gani ya kuongeza ajira kwa vijana?

Jibu: Mikakati ya serikali ya ajira kwa vijana ipo mingi, kwanza kwa kuyatambua makundi maalum kama vile wasanii, wajasiriamali na wakulima. Kazi kubwa ya serikali ni kuyarasimisha makundi hayo, pili kuwawezesha fedha za mitaji, mikopo ili wafanye kazi za kujiajiri. Siyo lazima mtu aajiriwe ofisini, serikali itaangalia jinsi ya kuwawezesha kujiajiri. Utaanzishwa mfuko wa vijana na Baraza la Uwezeshaji na tutawaomba wafadhili mbalimbali kama vile Plan International kusaidia kutoa mikopo na mitaji.

Ni changamoto gani nzito umekumbana nazo kwenye wizara yako tangu uteuliwe?

Jibu: Changamoto kubwa ni ya kupata ajira 4,400,000 ifikapo mwaka 2021 Pia tuna mkakati wa kukuza ujuzi nchini mpango ambao upo hadi mwaka 2021, hapa tunampango wa kuwapeleka vijana Veta wale wanaojua kutengeneza vitu mbalimbali ili watambuliwe rasmi na waongeze ujuzi na baadaye wajiajiri. Hii ni changamoto kubwa kwa sababu vijana wana maratajio juu yangu kuwasaidia kwa sababu ni kijana mwenzao. Changamoto nyingine ni migogoro sehemu za kazi inayotokana na waajiri kutotimiza sheria ya kazi ya mwaka 2015 licha ya kupitishwa sheria namba 15 na Bunge letu tukufu. Changamoto nyingine ni wageni kuja nchini na kufanya kazi ambazo zinaweza kufanywa na Watanzania.Waajiri wamekuwa wakitoa taarifa za uongo kuhusu wageni. Kwa mfano wanaweza kusema mgeni katoka nje ni injinia, akiingia kazini kumbe siyo, utamkuta ni afisa uhusiano. Tumeimarisha ukaguzi na tayari tumeondoa wengi kuwarudishwa makwao baada ya kuwabaini.

Kuna madai kwamba kuna Wachina wameajiriwa kufanya kazi ambazo zinastahili kufanywa na Watanzania. Je hilo likoje?

Jibu: Kama nilivyosema awali, sasa tumeimarisha ukaguzi na huwa tunapata taarifa za watu hao kutoka kwa raia wasamaria wema na idara ya uhamiaji na tunawakamata. Kwa mfano, kuna Mchina mmoja niliwahi kumkamata aliletwa nchini kwa kazi ya kufunga viti, huyu ni sawa na Mmachinga tu. Nilimtimua nchini siku hiyo hiyo. Niseme tu kwamba tumeongeza ukaguzi na kwa ushirikiano huo, tutawabaini kirahisi. Kinachosikitisha ni kwamba kuna baadhi ya Watanzania wanawaficha watu kama hao, nawasihi wasifanye hivyo na badala yake watoe taarifa serikalini tuwashughulikie.

Zile shilingi milioni 50 zitakazotolewa kwa kila kijiji kama alivyoahidi Rais Dk. John Pombe Magufuli, serikali ina utaratibu gani wa kuzigawa kwa Jiji la Dar es Salaam?

Jibu: Ni kweli Mheshimiwa Rais Magufuli alitoa ahadi hiyo nia ikiwa kukifanya kila kijiji kujaribu kukuza uchumi wake ili wanakijiji nao waone wana fursa ya kujiletea maendeleo. Kwa mfano vijiji vya Dodoma tuvifahamu kwa kulima zabibu, Babati ifahamike kwa ukulima wa ngano, Mtwara ifahamike kwa kulima korosho na kadhalika. Utaratibu wa kugawa fedha hizo unaratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu muda ukifika tutajua utaratibu utakaotumika siyo kwa Jiji la Dar es Salaam tu bali nchi nzima na tutawatangazia wananchi.

Itaendelea wiki ijayo.  

 

Leave a Comment