×

Tatizo la mimba kutoka (Recurrent Pregnancy Loss)

pregnant-womanMimba kutoka mara kwa mara ni tatizo linalotokea kwa wajawazito ambao mara zote wanakumbwa wakiwa na mimba yenye umri wa chini ya wiki 20 na zikawa zimetoka mara tatu au zaidi.

Mimba hizo zinazotoka kitaalam huitwa Recurrent Miscarriage au Recurrent Pregnancy Loss, tatizo hili huongezeka kadiri umri wa mwanamke unavyoongezeka.

Kuna sababu nyingi za mimba kutoka mara kwa mara kama vile matatizo ya mji wa mimba ya kuzaliwa nayo. Kizazi huwa hakina umbo au nafasi ya kutosha kuruhusu mtoto akue mpaka kuzaliwa.

Sababu nyingine ni mjamzito kuwa na vivimbe vya mji wa uzazi na shingo ya uzazi kulegea kitaalam huitwa Cervical Incompetence. Kadiri mimba inavyokua, shingo ya uzazi hushindwa kuhimili, hivyo mimba hutoka.

Tatizo lingine ni kushikana kwa kuta za mji wa mimba au kuwa na kisukari au ugonjwa wa vivimbe vya Ovary ama kuwa na upungufu wa homoni ya tezi ya shingo na mjamzito kuwa na ugonjwa wa Thrombophilia.

DALILI

Mara nyingi tatizo hili hutokea hasa mimba ikiwa bado changa, dalili zikijionesha wiki ya 10 au kuendelea kidogo. Mimba inayofuata kuharibika huwa katika wastani wa umri uleule wa mara ya kwanza au chini ya hapo kidogo.

Dalili kuu huwa ni kutokwa na damu ukeni, mjamzito kusikia maumivu ya tumbo hasa chini ya kitovu na kiunoni na mara nyingine kutoa uchafu au sehemu ya mimba iliyoharibika, homa na kutapika.

Unapopata dalili zinazoashiria tatizo hili wahi uonane na daktari atakayekufanyia uchunguzi na vipimo.

MATIBABU

Baada ya vipimo na uchunguzi na chanzo cha tatizo kujulikana, mgonjwa anaweza kutibiwa kisha tatizo likaisha. Matibabu yanaweza kuhusisha, dawa, upasuaji na kushona shingo ya uzazi kama imelegea Cervical Cerclage.

Leave a Comment