Wananchi wilayani Korogwe, Mkoa wa Tanga wamezua tafrani kufuatia kulalamikia mchakato wa ugawaji wa vyandarua vya msaada vilivyotolewa na serikali wakidai kuwa umegeuzwa mradi wa watendaji wasio waaminifu serikalini.
Wananchi hao waliozungumza na Uwazi walisema ugawaji huo uliofanyika maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo umekuwa kero kwao kwani kuna kaya ambazo ziliandikisha watu sita au saba lakini zikaambulia mgawo wa vyandarua viwili, hivyo kutojua jinsi ya kuvitumia katika familia zao.
Khadija Mwaimu alipohojiwa alikuwa na haya ya kusema: “Licha ya hayo ya wanafamilia kugawiwa vyandarua pungufu, kuna kaya ambazo hazikupata hata chandarua kimoja kiasi cha kuona kwamba Serikali ya Magufuli imewatenga.”
Naye Onesmo John alidai kuwa ugawaji wa vyandarua hivyo umevurugwa makusudi na baadhi ya watendaji wa serikali wasio waaminifu, hivyo kuwapa mwanya wa kuvificha na kuviuza kwa wafanyabiashara au kwa wananchi wasiokuwa na uelewa wa msaada huo.
Akijibu tuhuma hizo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, Abeid Mohammed alisema tayari kuna makubaliano kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya, Hafsa Mtasiwa (pichani) kwamba vyandarua vilivyobaki visambazwe kwa wananchi waliokosa.
“Katika Wilaya ya Korogwe kuna mahitaji makubwa ya vyandarua kwa wananchi wake wakiwemo wale wenye kadi ambazo walikosa kupatiwa bidhaaa hizo, lakini vipo ambavyo vimebaki,” alisema mkurugenzi huyo.
Hata hivyo, kiongozi huyo aliwaomba wajumbe wa baraza la madiwani kusaidia kuwabaini wale wote waliochukua vyandarua kinyemela ili wachukuliwe hatua kali za kisheria.
