Tunamalizia makala yetu kuhusu ugonjwa wa U.T.I baada ya kuanza kuelezea wiki iliyopita. Kwa kiasi kikubwa tatizo hili huathiri wanawake zaidi kuliko wanaume, zaidi ya mara mbili kwa kukadiria. Karibu kila mwanamke katika maisha yake anaweza kupata ugonjwa huu. Pia uwezekano upo kwa tatizo kujirudia mara kwa mara.
U.T.I yaweza kusababishwa na vijidudu vya namna nyingi. Mathalani ni vimelea (bakteria) japo pia na jamii nyingine ya vijidudu vinaweza kusababisha. Bakteria aina ya Escherichia Coli kwa kiasi kikubwa ndiyo wanaosababisha maradhi haya kama tulivyoona wiki iliyopita japo pia bakteria wengine wapo. Vijidudu hivi vyaweza kuingia katika njia ya mkojo kutokea nje ya mwili au hata kwa kupitia damu ya mhusika.
Kwa wanawake, fangasi katika sehemu za siri wamekuwa ni tatizo kubwa sana. Uwepo wa fangasi hasa kwenye uke na maeneo jirani pia huweka mazingira ya mvuto kwa bakteria kuvamia maeneo hayo na kuleta maradhi kama ya U.T.I.
Kwa wanaume mara nyingi kutokana na maumbile yao na mfumo mzima wa mkojo na viungo vyake, huwa siyo waathirika wakubwa wa U.TI. japo nao hupata.
Sababu hatarishi Risk Factors za U.T.I zipo nyingi, kulingana na umri, jinsia na mazingira ya mhusika. Vilevile ngono, tena ya mara kwa mara ni moja ya sababu zinazoweza kuchangia mtu kupata ugonjwa kwani bakteria waliopo katika sehemu za siri za mhusika vinaweza kupata nafasi ya kupenya na kuingia katika mfumo wa njia ya mkojo kwa urahisi zaidi.
Sababu nyingine ni upungufu wa kinga mwilini kwa sababu yoyote, ikiwamo ujauzito kwa wanawake na ugonjwa wa kisukari Diabetes. Lakini pia, sababu nyingine kadha wa kadha zinazosababisha upungufu wa kinga mwilini.
Dalili zinaweza kuwa kusikia maumivu wakati wa kukojoa, homa na maumivu katika viungo vya mkojo, kuhisi kuhitaji kukojoa mara kwa mara na pia mkojo kuwa na hali ya kuunguza wakati wa kukojoa, maumivu ya tumbo chini ya kitovu na au mgongo kwa chini. Mkojo wenyewe unaweza kuonekana wenye damu au usaha. Kwa watoto dalili pekee kubwa ni homa. Hii inaweza kuambatana na kushindwa kula vizuri, kulialia sana na hata kutapika.
TIBA NA USHAURI
Matibabu ya U.T.I yapo. Utaratibu mzima wa matibabu hutegemea majibu ya maabara, kisababisho cha maradhi na umri wa mhusika. Lakini unaozuilika kwa kuzingatia kanuni za afya bora hasa ya mwili na mazingira. Watu wanashauriwa kunywa maji mengi ili kupata mkojo mwingi ili pengine uweze kusafisha njia ya mkojo. Inashauriwa pia kukojoa mara tu baada ya tendo la kujamiiana. Kwa watoto ni muhimu kuzingatia matumizi sahihi ya pampers hasa kubadilisha kwa wakati.
MWISHO
Dk. Morise anapatikana Morise Dispensary, njia panda ya Mabibo mkabala na kituo cha mafuta.