LEO ndiyo leo asemaye kesho mwongo. Mshindi wa Bahati Nasibu ya Shinda Nyumba atajulikana saa kumi kamili jioni hii, baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Paul Makonda kufanya vitu vyake katika Viwanja vya Zakhem, Mbagala jijini Dar es Salaam.
Hii itakuwa ni katika kuhitimisha miezi sita ya bahati nasibu hiyo iliyoendeshwa na Kampuni ya Global Publishers kwa lengo la kurejesha sehemu ya mapato yake kwa jamii kupitia magazeti yake ya Championi, Uwazi, Ijumaa, Risasi, Ijumaa Wikienda na Amani.
Licha ya mshindi wa droo kubwa kupata zawadi ya nyumba, ambayo ni historia katika bahati nasibu zilizowahi kutolewa na kampuni za magazeti, pia kulikuwa na droo zingine ndogo nne ambazo washindi walijipatia zawadi kibao, zikiwemo pikipiki mbili, tv flat screen moja.
Nyumba hiyo yenye thamani ya mamilioni ya shilingi, imejengwa Salasala, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam na kwa mshindi, hana sababu ya kwenda na fenicha katika siku yake ya kwanza, kwani ina samani tayari ndani yake, tena za kisasa.
Meneja Mkuu wa Global Publishers, Abdalah Mrisho alikuwa mstari wa mbele kuhakikisha mjengo huo unamalizika kwa wakati na katika ziara yake ya mwisho wiki mbili zilizopita, aliwahakikishia wasomaji kuwa kila kitu kipo tayari na anayesubiriwa ni mshindi ili apewe ili maisha yaendelee.
Na mwanzoni mwa wiki hii, mastaa kadhaa wa Bongo Muvi na Bongo Fleva, walifanya ziara ya kuishuhudia nyumba hiyo ikiwa kamili ambao walieleza kufurahishwa kwao na uamuzi wa Kampuni ya Global Publishers kutoa nyumba hiyo ya kisasa kwa wasomaji wao, kwani ni jambo ambalo siyo rahisi kufanywa na kampuni zingine.
“Ni bonge la jumba aisee, ya kisasa hasa. Ninachoomba mimi, ingawa hii ni bahati ya mtu, lakini ningependa apate mtu maskini kabisa, asiye na kitu ili lengo la kampuni liwe limetimia,” alisema msanii wa muziki na filamu, Zuwena Mohammed ‘Shilole’ aliyekuwa mmoja wa mastaa waliokwenda kuishuhudia nyumba hiyo.
Kwa mujibu wa Meneja Mrisho, kutakuwa na burudani za jukwaani zitakazopamba shughuli hiyo ambayo itaanza saa tisa alasiri na kufikia tamati yake saa kumi, ambapo mgeni rasmi, Paul Makonda ataingia kazini kuifukunyua kuponi moja, itakayompatia mtu umiliki wa nyumba ya mamilioni jijini Dar es Salaam.
Katika meza kuu, kutakuwepo pia maofisa kutoka Bodi ya Taifa ya Michezo ya Kubahatisha, ambao ndiyo wasimamizi wa bahati nasibu zote halali zinazoendeshwa nchini. Kwa wakazi wa jirani na eneo la tukio, hii siyo shughuli ya kukosa ili kuwa shahidi wa tukio hilo la kihistoria.
