×

Usiku wa Sikinde na Msondo… hatoki mtu Idd Mosi hii, Dar Live

sikindeSikinde

Makala: Elvan Stambuli

BAADA ya kusubiriwa kwa hamu na mashabiki wa burudani, hatimaye imewadia ambapo bendi kongwe ya Muziki wa Dansi, Mlimani Park Ochestra ‘Wana Sikinde Ngoma ya Ukae’ chini ya Hassan Rehani Bitchuka ‘Super Sterio’ wanatarajiwa kukutana na wakongwe wengine kutoka Msondo Music Band chini ya Shaban Dede ‘Kamchape’ katika bonge moja la shoo, Idd Mosi hii ndani ya Uwanja wa Taifa wa Burudani, Dar Live uliopo Mbagala-Zakhem jijini Dar.

msondoMsondo

Burudani kwa watoto

Akizungumza na Risasi Vibes, Meneja wa Dar Live, Juma Mbizo alisema kuwa mapema kuanzia asubuhi kutakuwa na burudani kwa watoto ambapo watapata nafasi ya kucheza michezo mbalimbali.

“Pazia la burudani katika sikukuu hii ya Idd litafunguliwa mapema kuanzia saa mbili ambapo watoto wote watajumuika katika kucheza michezo mingi kama vile kuruka kamba, kuteleza, kubembea, kuogelea na mingine mingi ambapo kila mtoto ataondoka na zawadi kemkemu. Pia kutakuwa na kundi la sarakasi na kudansi la Wakali Dancers ambao siku hiyo watatoa burudani kwa watoto mwanzo mwisho,” anasema Mbizo.

Sikinde ndani

Mbizo alisema kuwa pazia la wakubwa siku hiyo litafunguliwa mapema kuanzia saa moja kwa burudani kibao.

“Wale wapenzi wa burudani tutakuwa na Bendi ya Sikinde itakayoonesha umahiri mkubwa sambamba na kuwapa mashabiki wao wimbo unaotamba sasa wa Jinamizi la Talaka unaopatikana katika albamu yao mpya iliyo na vibao nane.

“Usiku huu pia utapambwa na nyimbo zote za zamani zikiwemo Kasimu wa Kustarehe, Selina, Talaka Rejea, Tui la Nazi na nyingine nyingi huku Hemba akisaidiana na wapiga gitaa mahiri, Mjusi Shemboza, Kaingilila Maufi, Tony Bass na mpiga tumba Ally Jamwaka huku drums zikipigwa na Habib Jeff.”

MSONDO NAO NDANI

Mbizo aliongeza kuwa mbali na Sikinde, usiku huu utafunikwa pia na Msondo Music Band wakiwa na wanamuziki mahiri kama vile Roman Mng’ande ‘Romario,’ Salehe Bangwe, Huruka Uvuruge na mzee mzima Said Mabera.

“Mashabiki watarajie kuwasikia Msondo wakiwa na nyimbo kibao kuanzia Kicheko, Mawifi Mnanionea, Ndoa Ndoana, Nimezama Katika Dimbwi, Mti Mkavu na Mizimu.

“Nyimbo nyingine zitakazotikisa siku hiyo ni pamoja na Wabakaji, Tabu, Pricila, Penzi la Mlemavu, Piga Ua Talaka Utatoa, Tuma, Wapambe, Asha Mwana Sefu, Ajali, Mtanikumbuka, Barua ya Kusikitisha, Mwana Mkiwa, Kalunde, Kaza Moyo, Jesca, Kwenye Penzi, Binti Maringo na nyingine nyingi.”

Mbizo alimaliza kwa kusema kuwa kiongozi mwingine wa Msondo, Saidi Mabera ataongoza safu ya wapiga gitaa la solo na Rhythm ambao ni Ridhiwani Pangamawe na Huruka Uvuruge, Ramadhani Zahoro Bangwe na Mustafa Hamis ‘Pishuu’.

“Hivi utakosaje labda! Maana kwa upande wa gitaa zito la besi watakuwepo Ally Lindunga na Saad Ally ‘Sure Boy’ na drums litachanganywa na Saad Ally ‘Mashine’ na Arnold Kang’ombe, tarumbeta zitapulizwa na kijana machachari Roman Mng’ande na Hamis Mnyupe. Dorice George atapiga tumba, drums atazikung’uta Amiri Said Dongo,” aliweka nukta Mbizo.

Mbali na wakali hao, kwa upande wa Mchiriku kutakuwa na Msaga Sumu huku Taarab akisimama Bi Mwanahawa na kiingilio kitakuwa Sh. 7,000.

Leave a Comment