Wakazi wa Jiji la Dar wakiwa kwenye Ufukwe wa Coco ambako wengi huenda katika kusherehekea sikukuu mbalimbali.
STORI: MWANDISHI WETU, IJUMAA
DAR ES SAALAM: Msichana mmoja ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja, juzi kwenye Sikukuu ya Idd Mosi alinusurika kubakwa baada ya kulewa tilalila.
Msichana huyo mwenye umri kati ya 19 na 20 alikumbwa na balaa hilo baada ya kutinga kwenye ufukwe wa Coco Beach jijini Dar kisha kufakamia bia kisha kutaka kwenda kupiga mbizi.
Shuhuda aliyekuwa eneo la tukio, alisema kuwa, msichana huyo aliyekuwa amevalia kihasara alifika eneo hilo mida ya saa 10 akiwa peke yake, akaketi nje ya ukumbi uliopo eneo hilo la ufukwe kisha kuanza kuagiza bia.
“Alikunywa sana, baadaye wakaja vijana wawili walioonesha kumjua, wakamsalimia na kumchukua na kwenda naye kwenye maji. Waliogelea sana huku yule dada akionekana hana uzoefu na ile pombe ndiyo ikawa balaa, wakawa wanamshikashika na baadaye wakatoka kwenye maji na kuelekea kwenye mapango.
“Kule ndiko walikotaka kumfanyia kitu kibaya, alikuwa kalegea halafu nguo aliyokuwa amevaa ilikuwa hatari kwake. Wakati vijana wale wakimvutia kwenye kigiza ndipo walinzi wa eneo hilo walimuokoa na kumpa msaada,” alidai mtoa habari huyo.
Mpaka shuhuda huyo anaondoka eneo la tukio, mdada huyo alikuwa akitafutiwa usafiri wa kumfikisha kwao kwani alijieleza kwa tabu kuwa anaishi maeneo ya Kinondoni Mkwajuni jijini Dar.
Siku za sikukuu hasa maeneo ya mijini kumekuwa kukitokea matukio mengi mabaya ikiwemo baadhi kupotelewa na watoto, ajali pamoja na wizi ambapo familia zimetakiwa kuwa makini kuhakikisha sherehe hizo zinapita bila kuacha majonzi.