BAADA ya kutoa wimbo mmoja na kushindwa kuendelea na muziki, msanii wa filamu Bongo, Salma Jabu ‘Nisha’ ameibuka na kusema licha ya kuupenda sana muziki na uko kwenye damu ameamua kuuenzi kwa upromota.
Akipiga stori na gazeti hili, Nisha alisema kutokana na kushindwa kuendelea na muziki kwa sasa ameamua kuendelea kuuenzi kwa kuandaa shoo mbalimbali mikoani ambapo pamoja na hilo huwa anawapa burudani live mashabiki zake kwa uigizaji wake hali inayosababisha kuwa karibu nao zaidi.
“Nafanya filamu pia napenda sana muziki, tulifanikiwa kutoa wimbo mmoja na Flora Mvungi lakini sikuweza kuendelea tena hata hivyo nimeamua kuuenzi kwa namna nyingine ili kipaji changu kisiishie hewani,” alisema Nisha.
