×

Kichuya Atua Simba Kifalme

CgUal2wUIAECNIo

Shiza Kichuya.

Richard Bukos, Dar es Salaam

UONGOZI wa Klabu ya Simba, jana ulikata mzizi wa fitna na kuwatambulisha wachezaji wake  wapya kuelekea msimu wa 2016/17, ikiwemo kuwafanyia dua.

Hayo yalifanyika jana asubuhi kwenye Makao Makuu ya Simba, Mtaa wa Msimbazi, Kariakoo jijini Dar es Salaam ambapo hafla hiyo iliongozwa na Rais wa Wekundu hao, Evans Aveva, huku wachezaji wawili wapya kikosini hapo, Shiza Kichuya kutoka Mtibwa Sugar na Blagnon Fredric raia wa Ivory Coast wakipata mapokezi tofauti na wenzao.

Kichuya ambaye ni kiungo mshambuliaji alipata shangwe nyingi kila alipokuwa akipiga hatua mara baada ya kufika klabuni hapo ambapo aliwaonyesha Wanasimba yeye ni mwekundu kwa kuvaa vitu vingi vyenye rangi hiyo.

Kichuya alikuwa amevaa fulana nyeupe yenye mistari ya rangi nyekundu na pia alikuwa amebeba begi jekundu, hali ambayo ilisababisha shangwe ziwe nyingi alivyokuwa akipita katikati ya mashabiki hao waliokuwa wamejazana nje ya jengo hilo.

Mara baada ya kufika katikati ya mstari wa walipokuwa wamejipanga mashabiki hao, Kichuya alianza kutabasamu huku baadhi yao wakitaka kumvuta kupiga naye picha lakini ilibidi memba wa klabu hiyo waliokuwa wakiratibu shughuli hiyo kuwazuia kumvuta mchezaji huyo ambaye alikuwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu Bara mwezi Machi, mwaka huu.

Upande wa Blagnon, alipata shangwe lakini siyo kubwa kwa kuwa mashabiki wengi walionekana kutomtambua kwa sura na hivyo kujikuta muda mwingi wakimshangaa na kuulizana juu ya mchezaji huyo.

Katika shughuli hiyo ambayo iliendana na dua ya saa moja kuanzia saa tano asubuhi mpaka saa sita, ikiongozwa na mashehe na maustadhi, Simba ilitambulisha jumla ya wachezaji 10 wapya mbele ya mamia ya mashabiki na wanachama wa klabu hiyo waliojitokeza huku pia ikimtambulisha kocha mkuu wao mkuu, Joseph Omog.

Wachezaji wapya waliotambulishwa ni Jamal Mnyate, Emmanuel Semwanza waliotokea Mwadui FC, Kichuya, Mzamiru Yasin, Mohammed Ibrahim (wote Mtibwa Sugar) na Hamad Juma (Coastal Union), ambao hao wote wameshapewa mikataba.

Waliotambulishwa kuwa bado wapo kwenye majaribio na kwamba mambo yakienda vizuri muda wowote wanaweza kumwaga wino ni pamoja na Wacongo, Besala Bukungu na Moussa Ndusha, Blagnon na Mzimbabwe, Method Mwanjala.

Akizungumzia juu ya kinachoendelea Aveva ambaye alikuwepo eneo la tukio alisema: “Msimu ujao tutegemee mazuri kutoka kwa kikosi hiki ni wachezaji tuliowasajili kwa umakini wa kuzingatia vigezo na ubora wao, hata kwa kocha mkuu na benchi lake pia tuliwakabidhi timu baada ya kujiridhisha na uwezo na rekodi zao, tuwe na imani nao kuelekea msimu ujao.”

Baada ya hapo, kikosi cha Simba kikiwa na wachezaji 27 kiliondoka kuelekea Morogoro kuanza kambi ya wiki nne.

“Kambi yetu itakuwa ni mpaka Agosti 5, baada ya hapo tutaangalia mapendekezo yanasemaje,” alisema Aveva.

Ukiachana na Jonas Mkude anayetajwa kwenda Afrika Kusini kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa pamoja na Mzimbabwe, Justice Majabvi ambaye kurejea kwake klabuni hapo bado ni kitendawili, walioteuliwa kujumuishwa kambini hapo ni pamoja na Vincent Angban, Peter Manyika na Denis Richard.

Wengine ni Jamal Mnyate, Mohammed Hussein ‘Zimbwe’, Juuko Murshid, Emmanuel Semwanza, Novatus Lufunga, Abdi Banda, Method Mwanjala, Besala Bukungu, Awadh Juma, Said Ndemla, Hija Ugando, Musa Mgosi, Kichuya, Mzamiru Yasin, Ibrahim Ajib, Mohammed Ibrahim, Danny Lyanga, Moussa Ndusha, Hamad Juma, Peter Mwalyanzi, Baraka Yusuph, Blagnon Fredric, Hamad Juma na Mwinyi Kazimoto.

Leave a Comment