Watu huwa wanajiuliza kula matunda au juisi yake, nini bora?
Bora ni matunda kwani baadhi yake ngozi zake zinaweza kuliwa na ni chanzo muhimu cha virutubisho. Matunda hayo ni kama vile apple, blueberries, zabibu, strawberries, embe, pera, tango, zambarau na kadhalika.
Ngozi ya matunda hupokea mwanga wa jua na kutengeneza virutubisho vyenye rangi mbalimbali ambavyo ni muhimu sana kwa ujenzi na ulinzi wa afya ya binadamu.
Mfano wa virutubisho hivyo ni carotenoids na flavonoids ambavyo vinasaidia kuimarisha kinga na afya ya mwili kwa ujumla. Vitamin C inahitaji uwepo wa flavonoids ili kufanya kazi vizuri mwilini.
Ngozi ya matunda kama zabibu zinasaidia kulinda afya ya ngozi ya binadamu na kupunguza hatari ya mtu kupata ugonjwa wa saratani.
Ngozi na nyama za ndani za matunda kama machungwa ni chanzo kizuri cha nyuzi lishe, ambazo hupotea wakati wa kuchuja juisi.
Nyuzi lishe zinasaidia usagaji wa chakula tumboni, humwezesha mtu kupata haja kubwa na kuepuka saratani ya utumbo mpana. Zinapunguza pia kasi ya sukari kutoka katika utumbo na kuingia katika damu na zinapunguza wingi wa nishati.
Kwa hiyo nyuzi lishe zinachangia kupunguza hatari ya mtu kupata ugonjwa wa kisukari, unene na uzito kupita kiasi.
Ulaji wa matunda na mbogamboga unajaza tumbo na kumfanya mtu kujisikia ameshiba kwa muda mrefu. Juisi inaleta shibe ya muda mfupi na kuongeza nishati mwilini kwa haraka.
Ili kupata manufaa ya matunda na juisi asilia, watu wale matunda na mboga za majani aina tofauti kila siku. Pia, wanywe juisi asilia glasi moja kwa siku au kila baada ya siku mbili.
Tahadhari ni kwamba; imethibitishwa kisayansi kuwa unywaji wa juisi iliyoongezwa sukari iliyokithikiri unaweza kuchochea ugonjwa wa kisukari kwa wakubwa na watoto, unene na uzito kupita kiasi.
Katika mchakato wa kutengeneza juisi, baadhi ya virutubisho muhimu vinaharibika, vinapotea au vinaonekana kuwa ni uchafu na kutupwa.
Mtu mwenye matatizo katika kutafuna anapokunywa juisi ya asilia, anavipata virutubisho kwa wingi zaidi katika glasi moja japokuwa siyo sawa na aliyekula tunda ila ni kinywaji kizuri na kina faida kubwa kwa wagonjwa na wenye afya bora kwani inaongeza maji mwilini, inasafisha damu, inatoa sumu na vitu vingine vibaya mwilini kwa njia ya mkojo na humuepusha mtu kujenga mazoea ya kunywa soda au juisi za viwandani.