
Na Gabriel Ng’osha
Mpenzi msomaji ni Jumatatu nyingine murua ambayo mwenyezi Mungu ametujalia, hivyo hatuna budi kumshukuru kwa hilo. Bila kupoteza nukta ya muda, leo tujikite moja kwa moja kwenye mada yetu kama kichwa chake kinavyojieleza.
Ni ukweli ulio wazi kwamba, hakuna mtu anayependa kuachwa na mpenzi wake anayempenda, lakini kuna wakati inatokea, iwe kwa wewe mwenyewe kuwa chanzo au mwenza wako. Na kama kwa upande wako umefikia wakati huo wa kuachwa, basi jitahidi kuukubali ukweli ili maisha yasonge, japokuwa najua ni hali ngumu mno inayoambatana na maumivu ila unaweza, kama utanuia kuondokana na mateso hayo ya kuachwa.
Ninachotaka kukuambia leo katika somo hili ni hiki, unapoachwa na mpenzi wako, hicho ndicho kipindi cha wewe kufanikiwa kama utaukubali ukweli na kuamua kufanya kazi. Kwa kufanya kazi kwa bidii, kutakufanya kuona kama kuachwa kwako ni sehemu ya changamoto ya kukufikisha katika malengo uliyonayo hasa mafanikio ya kimaisha.
Katika hali kama hiyo, unaweza kufanikiwa kama utachukulia kuachwa kwako kuwa ni kwa sababu pengine huna elimu, fedha, uzuri, nyumba, gari au kazi nzuri, hata kama umeachwa lakini vitu hivyo unavyo.
Cha kufanya, akili yako ichochee kuona kama umeachwa kwa sababu huna elimu, basi uchungu huo utakufanya ukasome kwa bidii. Kama ulikuwa kweli hujasoma au kama elimu yako ilikuwa ni ndogo, basi ukaiongeze. Namaanisha kama uliishia kidato cha nne, ukaongeze kidato cha sita hadi chuo kikuu.
Ujichochee mwenyewe katika akili yako, kama umeachwa kwa sababu huna fedha, basi uongeze bidii katika kufikiria namna ya kutengeneza fedha nyingi na mwisho wa siku, ufanikiwe kupitia changamoto hiyo.
Cha msingi usijenge chuki kwa mtu aliyekuumiza kwa sababu ya kukuacha, bali ona kama ni fursa ya kuchomoka kimaisha.
Najua unaumia kwa sababu uliamini ndiye mume au mke wa ndoto zako, lakini leo kakupiga chini, tena kwa sababu isiyo na msingi.
Umia tu, sawa, lakini nataka kukuambia kuwa yawezekana mlikutana ili iwe kama ni daraja la wewe kwenda kukutana na mtu ambaye ndiye hasa anayestahili kuwa mume au mke wako bora na wa maisha.
Hata hivyo, kwa akili ya kibinadamu na kutokufikiria, unaweza ukahisi una mikosi kwa kuona mpenzi unayekuwa naye anakuacha, lakini amini kuwa huna mikosi wala hujalogwa. Kinachotokea ni kwamba tu labda hutaki kuukubali ukweli kuwa huyo alikuwa ni sehemu ya kivuko chako ili uende ng’ambo nyingine yenye mafanikio.
Mpenzi msomaji usikose sehemu ya pili ya mada hii wiki ijayo. Kwa ushauri na maoni, tembelea ukurasa wetu wa Mimi na Uhusiano kwenye Mtandao wa Kijamii wa Facebook, Insta: mimi_na_uhusiano, Twitter:miminauhusiano au jiunge na Group la M&U la WhatsApp kupitia namba 0657486745 ili kupata mengi zaidi.