×

Karama Akiri Ndoa Yake Kuvunjika

  STORI: WAANDISHI WETU | RISASI MCHANGANYIKO| DAR ES SALAAM

Msanii mkongwe wa muziki wa kizazi kipya, Luteni Karama, aliyetamba na kundi la Gangwe Mob, amekiri kuwa ndoa yake na Aisha Yassin, iliyofungwa Mei mwaka jana, ina mushkeli, Risasi Mchanganyiko lina mkasa mzima.

Awali, chanzo cha kuaminika kilieleza kuwa wawili hao wametengana, baada ya kutokea kutoelewana baina yao, kitu kilichomfanya mwimbaji huyo kuondoka nyumbani kwao mkewe Magomeni na kurejea alikokuwa akiishi mwanzo, Tabata.

Inadaiwa kuwa tangu ifungwe, ndoa hiyo imekuwa na misukosuko na haijawahi kuwa na utulivu kwani kabla ya kuvunjika, Karama aliwahi kumuacha mkewe ndani na kuhamia kwa mpenzi wake wa zamani, Isabela Mpanda ambapo baadaye alirudi tena kwa mkewe huyo.

Karama na mkewe siku ya ndoa yao.

“Tangu Karama afunge ndoa na Aisha ambaye alikuwa rafiki wa Isabela, hawajawahi kuwa na amani kwenye ndoa hata kidogo, imekuwa ya misukosuko mpaka hivi ilivyovunjika na Karama amerudi Tabata alikokuwa akiishi kabla ya kuoa na kuhamia kwa mwanamke huyo,” kilisema chanzo hicho.

Ili kuleta usawa wa habari Risasi Mchanganyiko lilimtafuta Karama ambaye alikiri ndoa yake kuvunjika na kurudi Tabata alikokuwa akiishi zamani huku akisema hana mpango wa kuoa tena wala kurudiana na mwanamke wake huyo kwa sasa.

Waalikwa wakipiga mpunga siku ya harusi yake.

“Ni kweli ndoa imevunjika, mwanamke muongomuongo haeleweki utaishi naye vipi, na mwanamke wa hivyo mtakuwa mnajenga familia au mnabomoa, siwezi kuwa na mwanamke asiyekuwa na malengo, sasa hivi najipanga kurudi upya kwenye muziki,” alisema Karama.

Aisha hakuweza kupatikana kupitia simu yake ya mkononi ili azungumzie kwa upande wake, kwani mara zote simu yake haikupatikana. Hata hivyo, juhudi za kumtafuta zinaendelea.