The House of Favourite Newspapers

Aliyemburuza Ali Kiba Mahakamani Apasua Jipu!

DAR ES SALAAM: Jipu pwaa! Siku chache tangu amburuze mahakamani staa wa muziki wa Bongo Fleva, Ali Saleh Kiba ‘King Kiba’ kwa kesi ya madai ya matunzo ya mtoto, mwanamama mfanyabiashara maarufu jijini Dar, Hadija Hassan (pichani) ameibuka na kupasua jipu, Risasi Mchanganyiko linakupa habari kamili.

TUJIUNGE NA CHANZO

Habari kutoka kwa chanzo makini kilicho karibu na familia ya Kiba zilidai kuwa, mwanamama huyo ambaye ni mzazi mwenza wa Kiba alipatwa na hasira baada ya kusikia msanii huyo anaoa hivyo akaamua kwenda kumchukua mtoto wake ambaye alikuwa anaishi na baba yake huyo.

“Unajua huyo Hadija alianza figisufigisu mara baada ya kusikia Kiba yupo kwenye maandalizi ya ndoa ndipo akaanza kudai mtoto na kwenda kumchukua kwa nguvu nyumbani kwa akina Kiba alikokuwa akiishi maeneo ya Kariakoo jijini Dar.

“Sasa hapo ndipo ugomvi ulipoanza kwa kuwa hakupendezwa na kitendo hicho cha Kiba kumuoa mwanamke mwingine na hakuwa tayari kuona mwanaye akilelewa na mama wa kambo. Yaani kitendo cha Kiba kuoa ndiyo sababu kubwa ya haya yote,” kilidai chanzo hicho.

Kiliendelea kusimulia kwamba, baada ya mwanamama huyo kumchukua mtoto wake ndipo Kiba aligoma kutoa matunzo, jambo lililomfanya Hadija aende Ustawi wa Jamii ambako nako ilishindikana ndipo suala hilo likahamishiwa mahakamani.

HUYU HAPA HADIJA

Kufuatia madai hayo, Risasi Mchanganyiko lilimtafuta Hadija na kuzungumza naye kwa njia ya simu kwa takriban dakika 30 ambapo alipopatikana alipasua jipu juu ya sakata hilo huku akieleza kuwa habari hizo siyo za kweli, bali ni uzushi tu na watu hawawezi kujua kilichoko kwenye familia za watu.

“Siyo kweli kwamba nilianza figisufigisu baada ya kusikia Kiba anaoa, bali niliamua kwenda kumchukua mwanangu kwa sababu nyingi sana. Hakuna anayeweza kujua na siwezi kuzungumza sana maana ni mambo ya kifamilia na familia zina mambo mengi sana.

“Isitoshe mwanangu bado ni mdogo hajafikisha umri wa miaka saba bado ndiyo maana nikaona ni vyema kukaa na mwanangu kwa kuwa nilikuwa siridhishwi na malezi aliyokuwa akipata, nikaongea na baba yake, nikamchukua mtoto wangu na hapo ndipo mambo yalipobadilika.

“Kuhusu mahakamani siwezi kuongea sana maana kila kitu kiko huko, siwezi kuingilia tena mambo ya mahakama ila nasisitiza kwamba sijafanya figisu kisa ndoa kama watu wanavyosema, bali siku nyingi tu nilishaanza kuhusu ishu ya kumchukua mwanangu,” alisema Hadija.

IKO HIVI

Kufuatia sakata hilo, Hadija alifungua kesi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar, akidai matunzo ya mtoto kwa mzazi mwenzake, Kiba.

NDOA YATIKISIKA

Kwa mujibu wa watu wa karibu na staa huyo wa Bongo Fleva, walieleza kuwa ndoa ya Kiba ambayo bado ni changa na haina hata mwezi tangu ifungwe, imekumbwa na mtikisiko mkubwa kutokana na kesi hiyo.

“Unaambiwa ndoa ya Kiba ambayo ndiyo kwanza ni changa kabisa, ina mtikisiko wa aina yake kutokana na suala hilo la kuburuzwa mahakamani ambapo kesi inatarajiwa kuanzwa kutajwa hivi karibuni, mke wa Kiba hamuelewi mumewe kabisa kutokana na ishu hiyo,” alidai mtoa ubuyu wetu.

KIBA ANASEMAJE?

Risasi Mchanganyiko lilimtafuta Kiba ili kujua anazungumziaje sakata hilo, lakini simu yake ya mkononi haikuwa hewani na alipotafutwa mmoja wa viongozi wa lebo yake hakuwa tayari kuzungumzia ishu hiyo.

TUJIKUMBUSHE

Aprili 19, mwaka huu Kiba alifunga ndoa ya kifahari na aliyekuwa mchumba wake wa muda mrefu, Amina Khaleef huko jijini Mombasa, Kenya na kufuatiwa na sherehe kubwa Aprili 29, mwaka huu iliyofanyika jijini Dar.

STORI: Gladness Mallya, Risasi Mchanganyiko

Comments are closed.