Baada ya Kushindwa Kufanya Shoo Kenya, Afya ya Diamond, Hofu Yantanda

HOFU imetanda juu ya afya ya staa wa Afro-Pop barani Afrika, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’, Amani limedokezwa.

 

TUJIUNGE NAIROBI, KENYA

Habari zimeeleza kuwa wikiendi iliyopita mwanamuziki huyo alishindwa kabisa kufanya shoo iliyokwenda kwa jina la Tomorrow’s Leaders Festival iliyoandaliwa na Bendi ya Morgan Heritage ya Jamaika iliyofanyika kwenye Uwanja wa Kasarani jijini Nairobi, Kenya kwa kile kilichoelezwa kuwa aliumwa ghafla.

 

Katika tamasha hilo zilishuhudiwa shoo nyingi kutoka kwa wanamuziki mbalimbali kutoka Kenya kama Wyre, Jua Cali, Naiboi na Femi One.

Nyingine zilikuwa za wanamuziki kutoka nchi mbalimbali kama Jose Chameleone kutoka Uganda, Stonebwoy wa Ghana, Stanley Enow wa Cameroon, Alaine kutoka Jamaika na Bendi ya Morgan Heritage ambayo ilikuwa ya mwisho kuangusha shoo matata.

 

‘TUNAMTAKA SIMBA’

Hata hivyo, katika hali ya sintofahamu, wanamuziki wengine wawili waliotarajiwa ‘kupafomu’ kwa mujibu wa matangazo walikuwa ni Diamond au Mondi kutoka Tanzania na Yemi Alade wa Nigeria. Wawili hao hawakuonekana hivyo kuibua tafrani ambapo mashabiki walikuwa wakiimba; “Tunamtaka Simba (Diamond)!”

Wakiwa stejini wakitoa burudani huku kelele za ‘kumtaka simba’ zikiongezeka, ilibidi mmoja wa wanamuziki wa Bendi ya Morgan Heritage aliyetajwa kwa jina la Peetah Morgan kueleza umati uliofurika Uwanja wa Kasarani juu ya kwa nini Diamond hakupanda jukwaani kufanya shoo?

 

‘DIAMOND HAJISIKII VIZURI’

“Naomba niwape udhuru kutoka kwa Simba (Diamond), hajisikii vizuri, lakini yupo hapa Nairobi. Mtu anapokuwa mgonjwa, lazima tumhurumie na kama unampenda Simba sema rasta,” alifafanua jamaa huyo na kuibua hofu ambapo mashabiki waliendelea kupiga kelele za; “Tunamtaka Simba!”

MENEJA WAKE ANENA

Hata hivyo, katika kuweka mambo sawa, mmoja wa mameneja wa Mondi, Sallam Sharif ‘SK’ au ‘Mendez’ alisema kuwa wangefafanua ishu hiyo kupitia kurasa za staa huyo za mitandao ya kijamii.

 

“Diamond atafafanua kile kilichotokea kupitia mitandao yake ya kijamii hivyo mashabiki wake wasijali,” alisema Sallam kupitia moja ya intavyuu alizofanya jijini Nairobi baada ya shoo hiyo. Kwa upande wake Yemi Alade naye ilielezwa kuwa alishindwa kupafomu kwa kuwa naye hali yake ya kiafya haikuwa nzuri.

 

SHOO ZA GEITA, KAHAMA ZATAJWA

“Hali ya hewa hapa (Nairobi) siyo nzuri. Diamond ametoka kwenye ziara yake kubwa (Geita na Kahama). “Yemi yeye aliugua ghafla, anaumwa,” alisema jamaa huyo wa Bendi ya Morgan Heritage ambao wamefanya kolabo na Diamond ya Wimbo wa Africa and Jamaica.

 

Mapema, wanamuziki wa Kenya walionekana wakiwa wamejikusanya sehemu moja wakiwa wamekasirika na hawakutaka kufanya shoo hadi baadaye sana iliposemekana kuwa walilipwakwanza chao ndipo wakakubaliana.

KUHUSU AFYA YA MONDI

Baada ya habari za Mondi kushindwa kupafomu kusambaa mitandaoni, kuliibuka maswali mengi ya kile kinachowezekana kumfika huku suala la afya yake kudhoofu katika siku za hivi karibuni likipewa kipaumbele.

 

Kwa mujibu wa watu waliomshuhudia Mondi kwenye shoo za Kahama na Geita, jamaa huyo alionekana kudhoofu (angalia picha ukurasa wa mbele) hivyo kuibua sintofahamu na ni nini hasa kinamsibu staa huyo.

 

Hata hivyo, mmoja wa madaktari maarufu jijini Dar, Dk Chale alilieleza Gazeti la Amani kile kinachoweza kuwa kimemsibu Mondi. “Moja, kama ulivyosema alikuwa kwenye ziara kubwa ya kimuziki ambapo alikuwa anafanya shoo ya peke yake (One Man One Mic) hivyo inawezekana alijiandaa sana kwa mazoezi magumu ndiyo maana akapungua mwili.

 

“Lakini kuhusu kuumwa ghafla akiwa Nairobi baada ya kutoka Kahama na Geita inawezekana ule ulikuwa uchovu kwa sababu ndani ya siku mbili alifanya shoo mbili kubwa za zaidi ya saa 8 kila siku hivyo muda wa kupumzika ulikuwa mdogo.

 

“Pili, kama unavyojua, Diamond amekuwa kwenye malumbano na mzazi mwenzake (Zarinah Hassan ‘Zari The Boss Lady’) juu ya kuwaona watoto wake. “Wewe fikiria mtu ambaye kila akikaa alikuwa anasema anawapenda watoto wake (Tiffah na Nillan) halafu ghafla tu anakosa fursa ya kuwaona tu achilia mbali kucheza na kufurahi nao kama baba mzazi.

 

“Unaweza ukaona ni kwa kiasi gani suala la wanaye linavyoweza kuwa limemsababishia msongo au stress kiasi cha kukonda. “Unajua watu wengi hawajui tu, lakini hakuna kitu kibaya kama stress kwenye maisha. Ukiacha kukonda, stress zinasababisha hata kifo.

 

“Mwisho, inawezekana kukonda kumesababishwa na labda mfungo maana ninavyojua Diamond ni Muislam mzuri hivyo alikuwa amefunga. “Sasa chukua mfungo, changanya na kufanya mazoezi mazito kwa ajili ya shoo halafu malizia na stress za wanaye, kukonda hakukwepeki.

NINI CHA KUFANYA?

“Mimi ninamshauri apate muda wa kutosha wa kupumzika kwa sababu mapumziko ni dawa binadamu. “Anapaswa kula vizuri kwani mwili wa binadamu unategemea chakula ili uweze kujiendesha kama vile gari linategemea nishati ya mafuta ili lifanye kazi.

 

“Pia anapaswa kupata muda wa ku-relax kama moja ya njia za kukabiliana na msongo,” alimalizia daktari huyo. Kwa sasa Mondi yupo kwenye mapenzi na Tanasha Donna ambaye naye ni mwanamuziki, video vixen na mtangazaji wa nchini Kenya anayeaminika kuwa ana jukumu zito la kuhakikisha jamaa huyo anarejea kwenye ubora wake.

 

HAMISSA Mobetto Kanumba Alikuwa….Kuhusu Tumbo Mmhh!!!

Loading...

Toa comment