The House of Favourite Newspapers

Balinya, Sibomana Wapewa Saa 120 Kuiua Zesco

KOCHA Mkuu wa Yanga, Mkongomani, Mwinyi Zahera, amesema kuwa ni suala la muda tu washambuliaji wake watafunga huku akitoa siku tano sawa na saa 120 au dakika 7200 za kuisuka safu hiyo ili kabla ya mchezo wa Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika wawe fiti.

 

Mkongomani huyo anaamini uwezo wa kila mshambuliaji wake huku akijipanga kutatua tatizo sugu la washambuliaji wake ambao wamekuwa wakishindwa kutumia vema nafasi wanazotengenezewa.

Safu ya ushambuliaji ya Yanga inaundwa na David Molinga, Patrick Sibomana, Sadney Urikhob, Maybin Kalengo na Juma Balinya.

 

Akizungumza na Championi Jumatatu, Zahera alisema kuwa bado anaendelea kuimarisha safu yake ushambuliaji ambayo anaamini itakaa sawa kabla ya mchezo wao wa Raundi ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika watakapopambana na Zesco ya Zambia Jumamosi hii Uwanja wa Taifa, Dar.

 

Zahera alisema kuwa tayari ameanza kuona mabadiliko kwenye mchezo wao wa kirafiki dhidi ya Pamba FC ya Mwanza ambao Molinga alifunga bao lake la kwanza Yanga katika sare ya bao 1-1, Uwanja wa CCM Kirumba.

 

Aliongeza kuwa anaanza kuona mabadiliko ya washambuliaji wake ambao katika mchezo huo licha ya kutotumia nafasi nyingi walizokuwa wanazipata, lakini walifanikiwa kufunga mabao, licha ya mengine kukataliwa na mwamuzi kwa kucheza ‘offside’.

 

“Katika mchezo wetu wa kirafiki na Pamba tulistahili kufunga mabao mengi, lakini umakini mdogo ukasababisha washambuliaji wangu wakashindwa kutumia nafasi hizo.

 

“Licha ya kukosa nafasi hizo lakini naanza kuona mabadiliko katika safu yangu ya ushambuliaji ambayo ni tofauti na michezo iliyopita, kwani walifunga bao moja lililokubaliwa na mwamuzi tofauti na mengine yaliyokataliwa kwa kuwa offside.

 

“Hivyo, ninaamini kwa siku hizi zilizobaki washambuliaji wangu watakuwa tayari wameshika mafunzo ninayoendelea kuwapa, kwani nimewaandalia programu maalum ya mazoezi ili kabla ya mchezo wetu na Zesco wawe tayari,” alisema Zahera.

WILBERT MOLANDI, Dar es Salaam

Comments are closed.