The House of Favourite Newspapers

Beki Lipuli apewa mikoba ya Zana Simba

BEKI wa kulia Simba, Zana Coulibaly huenda msimu huu ukawa wa mwisho ndani ya kikosi hicho baada ya uongozi wa timu hiyo kudaiwa kuwa katika harakati za kutafuta mbadala wake.

 

Hali hiyo inatokana na kila kinachodaiwa kuwa mchezaji huyo mwenye mbwembwe nyingi uwanjani kushindwa kuonyesha kiwango cha juu kilichosababisha akasajiliwa na timu hiyo.

 

Uongozi wa Simba, hivi sasa unadaiwa kuwa katika mazungumzo na wachezaji wawili wa Lipuli FC kwa ajili kwenda kuchukua nafasi hiyo ya Coulibaly.

 

Habari ambazo Championi Jumamosi limezipata kutoka ndani ya Simba zimedai kuwa uongozi wa unafanya mazungumzo na William Lucian ‘Gallas’ na Haruna Shamte ambao wote ni wachezaji wa Lipuli FC.

 

Wachezaji hao kwa pamoja wamewahi pia kuitumikia Simba kwa nyakati tofauti kabla ya kuondoka na kwenda kutafuta maisha sehemu nyingine.

 

“Mmoja kati ya wachezaji anaweza kusajiliwa kwa ajili ya kuchukua nafasi ya Coulibaly ambaye kunauwezekano mkubwa akaachwa.

 

“Atakayesajiliwa atakuja kusaidiana na Shomari Kapombe ambaye muda mwingi alikuwa nje ya uwanja akiuguza majeraha baada ya kuumia akiwa na kikosi cha Taifa Stars,” kilisema chanzo hicho cha habari.

 

Alipoulizwa Gallas kuhusiana na hilo alisema kuwa: “Ni kweli tetesi hizo hata mimi nazisikia ila bado sijazungumza na kiongozi yoyote ule wa Simba kuhusiana na ishu hiyo, ila ikitokea wakaja basi nitaangali nini cha kufanya sababu soka ndiyo kazi yangu.”

 

Naye Shamte alizuga kuwa: “Simba bado hawajaniambia chochote kuhusiana na ishu hiyo ila kuna baadhi ya timu kama vile Yanga wao ndiyo nishazungumza nao, hata hivyo wakija mimi sina tatizo kikubwa ni kipato.”

Sweetbert Lukonge, Dar es Salaam

Comments are closed.