The House of Favourite Newspapers

Benki Kuu ya Tanzania yawaka moto!

0

BOT (2)Jengo la Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Najuwa wajuwa, Lakini mimi nakujuza zaidi

ASUBUHI ya Julai 5, 1984, wakazi wa Dar es Salaam waliamka kwa mshangao baada ya kusikia na kuliona jengo la Benki Kuu ya Tanzania (BoT) likiwa linaungua kwa moto uliokuwa umesambaza moshi mkubwa na mzito juu ya anga la mji  huo ulio ufukweni mwa Bahari ya Hindi.

Tukio hilo lilitokea kiasi cha miaka 32 iliyopita, wakati wa utawala wa Mwalimu Julius Nyerere ambapo, kama kawaida, Watanzania waliokuwa na kazi na ambao hawakuwa na kazi,  walifurika maeneo jirani ya jengo hilo ambalo ndilo ‘mama wa fedha’ za nchi hii na kushuhudia likiwaka moto huku magari kibao ya zimamoto na wafanyakazi wake wakihangaika kuudhibiti.

Kama kawaida pia, majeshi ya usalama yalikuwa yamefurika eneo hilo ili kuhakikisha hapatokei purukushani yoyote wakati wa kupambana na janga hilo.

Kwa ufahamisho tu ni kwamba jengo lililoungua ni lile  ‘orijino’, yaani jengo la mwanzo kabisa la benki hiyo lililofunguliwa Julai, 1969 na Mwalimu Julius Nyerere. Ujenzi wa jengo hilo lenye ghorofa zipatazo sita  – wakati huo –  uligharimu Sh. milioni 11, ambazo zilikuwa ni sawa na Dola za Marekani milioni 1.6.

Kwa mahesabu ya sasa, si rahisi kuamini kwamba jengo kubwa kama hilo liligharimu kiasi kidogo cha pesa kama hicho!  Hata hivyo, ikumbukwe kwamba jengo hilo lilifunguliwa miaka ipatayo 47 iliyopita.

Hata hivyo, jengo hilo ambalo liliungua sehemu zote ‘laini’ na kubaki likiwa zima katika sehemu zote ‘ngumu’ kama vile kuta, zege na vyuma na kadhalika, lilikarabatiwa na kuanza kutumika, japokuwa lilifanyiwa mabadiliko kadhaa kwa ndani na nje.

Habari kamili au za wazi kuhusu chanzo cha moto huo na hasara zake, hazikutolewa wazi sana licha ya wapelelezi kutoka Uingereza ambao walikuja kufanya uchunguzi wa tukio hilo na kutoa ripoti kwa mamlaka husika.  Hata hivyo, ni dhahiri hati na kumbukumbu mbalimbali ziliteketea katika moto huo ambapo shughuli nyingi zilikuwa zinafanyika kwenye ‘makaratasi’.

Tofauti na taswira ya wakati huo, makao makuu ya benki hiyo hivi sasa yamebadilika sana, kwani jengo hilo lililoungua hivi sasa liko katikati ya majengo pacha marefu, kila moja likiwa na ghorofa 20,  ambayo yalikamilika kujengwa mwaka 2006.  Matokeo yake, majengo hayo mawili, kaskazini na kusini mwa jengo orijino, yamelifanya kuonekana kama ‘kambilikimo’ kenye kuchekesha.

Leave A Reply