
Mvutano kati ya Marekani na Iran umeendelea kupanda baada ya Marekani kukanusha madai kuwa meli yake ya kivita ilishambuliwa katika Strait of Hormuz, huku Rais Donald Trump akitangaza operesheni kubwa ya kijeshi kulinda meli zilizokwama katika njia hiyo muhimu ya biashara ya mafuta duniani.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Iran, jeshi lake lilidai kuwa lilizuia meli za kivita za Marekani kuingia katika eneo hilo na hata kudai kuwa moja ya meli hizo ilipigwa kwa makombora mawili. Hata hivyo, Kamandi ya kijeshi ya Marekani (CENTCOM) imekanusha vikali madai hayo, ikisema hakuna ushahidi wa tukio hilo kutokea karibu na pwani ya Jask kusini mwa Iran.

Hatua hii imekuja kufuatia tangazo la Trump la kuanza operesheni iitwayo “Project Freedom”, inayolenga kusaidia meli zilizokwama kupita salama katika mlango huo. Mpango huo unahusisha wanajeshi takribani 15,000 pamoja na zaidi ya ndege 100 za kijeshi za anga na baharini.
Trump amesema operesheni hiyo ni ya kibinadamu, ikilenga kuwaokoa mabaharia na wafanyakazi wa meli wanaokabiliwa na uhaba wa chakula na mahitaji muhimu, akiwaita waathirika wa mazingira. Hata hivyo, ameonya kuwa jaribio lolote la kuingilia operesheni hiyo litakabiliwa na nguvu.

Kwa upande wa Iran, viongozi wa juu wa kijeshi wameonya kuwa watachukulia hatua kali dhidi ya nguvu yoyote ya kigeni itakayojaribu kuingia au kukaribia eneo hilo. Meja Jenerali Ali Abdollahi amesema jeshi la Iran liko tayari kukabiliana na hatua yoyote ya kijeshi, hasa kutoka Marekani.
Wakati huo huo, mwanasiasa wa Iran, Ebrahim Azizi, ameonya kuwa uingiliaji wowote wa Marekani katika mfumo mpya wa usimamizi wa bahari wa Hormuz utachukuliwa kama uvunjaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano.
Kwa mujibu wa International Maritime Organization, zaidi ya mabaharia 20,000 na meli zaidi ya 2,000 bado zimekwama katika njia hiyo tangu kuzuka kwa vita mnamo Februari 28, hali inayozidisha wasiwasi wa kimataifa kuhusu usalama wa usafirishaji wa mafuta.
