Biteko Ahudhuria Uzinduzi wa Kituo cha Kujaza Gesi Asilia Kwenye Magari
Waziri Doto Biteko amehudhuria uzinduzi wa kituo cha kwanza cha kujaza gesi asilia na kubadili mfumo wa magari kutumia gesi Tanzania ambacho kitakuwa cha kwanza nchini Tanzania, kikijulikana kama ‘Master Gas’ ambacho kitakuwa na uwezo wa kuhudumia magari 800 kila siku.
Huu utakuwa ni miongoni mwa mfululizo wa vituo 12 vitakavyojengwa na TAQA Dalbit miaka ya hivi karibuni kwa jumla ya uwekezaji unaozidi dola Milioni 10 za Marekani.
Mpango huu unapanga kukuza matumizi ya gesi asilia kwa sababu ni nafuu kwa asilimia 50, mbadala safi ukilinganisha na mafuta ya kawaida.
TAQA Dalbit imezindua kituo cha kwanza cha Kujaza Gesi Asilia (CNG) kinachojulikana kama ‘Master Gas’ na cha kugeuza mfumo wa magari kinachopatikana Pugu barabara ya uwanja wa ndege jijini Dar es salaam Tanzania.
Mradi huu umeanzishwa na TAQA Dalbit kupitia ubia kati ya TAQA Arabia na JCG Oil & Gas katika jitihada za kuimarisha adhma ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania la kuongeza matumizi ya akiba yake ya gesi asilia, ambayo inatoa mbadala wa mazingira safi na unafuu kwa watumiaji.
Doto Mashaka Biteko, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati wa Tanzania, ambaye aliongoza hafla ya ufunguzi wa kituo hicho, aliwapongeza TAQA Arabia na JCG Oil & Gas kwa uwekezaji wao wa pamoja na kuiunga mkono serikali katika uwekezaji.
“Tuko kwenye jitihada za kuleta mabadiliko katika sekta ya nishati nchini. Kupitia maono ya viongozi wa sekta binafsi kama TAQA Dalbit, tunakaribisha ufumbuzi kwa nishati endelevu. Kituo kipya cha kujaza gesi asilia pamoja na cha kugeuza mfumo wa magari ya kawaida kuanza kutumia gesi ni mafanikio makubwa, pia inaonyesha uwezo wa kiteknolojia wa taifa letu na mustakabali wa baadaye katika mazingira na kiuchumi,” alisema Biteko.
Magari yanayotumia mfumo wa gesi asilia yanakadiriwa kutoa gesi ya kaboni dayoksaidi (CO2) chini ya asilimia 25, kwa wastani gesi asilia, ni nafuu kwa asilimia 50 ukilinganisha na mafuta ya kawaida hivyo kituo hiki cha kujazia gesi kwenye magari kitasaidia matumizi ya nishati safi ikiwa na kiwango kidogo cha kaboni na pia ni rafiki kwa mazingira.
Kituo cha gesi asilia kina uwezo wa ujazo wa kilo 11,000 cha gesi asilia (7600 sqm za ujazo wa gesi) yenye uwezo wa kuhudumia magari 800 kwa siku, wakati kituo cha kubadili mfumo wa magari kitakuwa na uwezo wa kuhudumia mpaka magari 1,000 kwa mwaka.
Kituo cha kubadili mfumo wa magari kitakuwa na uwezo wa kuhudumia magari ya aina zote kama vile ya abiria, ya matumizi mbalimbali, ya michezo, mabasi, na malori ya mizigo.
Kituo cha gesi asilia ni cha kwanza miongoni mwa 12 ambavyo TAQA Dalbit inatarajia kuvijenga miaka ya hivi karibuni nchini Tanzania kuunga mkono mikakati ya serikali katika kuongeza matumizi ya gesi asilia kama nishati safi mbadala na yenye gharama nafuu.
Akitangaza ufunguzi huo, Bi. Pakinam Kafafi, Mkurugenzi Mtendaji wa TAQA Arabia, amesema:
“Tunayo furaha kutangaza uzinduzi wa Kituo cha Kujaza Gesi Asilia cha Tanzania na cha kubadilisha mfumo wa magari Dar es Salaam.
Hii ni hatua kubwa kwa TAQA Arabia tunapoungana na JCG pamoja na serikali ya Tanzania, ikiwa ni juhudi muhimu katika dhamira yetu ya kuhudumia mahitaji ya nishati nchini huku tukiendana na dira ya nishati ya taifa.
TAQA Arabia, kinara wa utoaji wa huduma na mwanzilishi wa teknolojia ya nishati asilia, tunafurahi kuleta suluhisho hili la gharama nafuu na kirafiki kwa mazingira, kuimarisha ukuaji wa uchumi, na kupunguza uzalishaji wa hewa chafu.
Kwa ujuzi wake, na rekodi ya miradi ya nishati iliyofanikiwa, TAQA Arabia iko tayari kusaidia Tanzania katika kufaidika na hifadhi yake ya gesi na uwezo mkubwa wa nishati katika suluhisho bora, na endelevu. TAQA Arabia inatazamia pia kuongeza thamani kwa wateja na usambazaji wa gesi asilia, uzalishaji wa kawaida na mbadala wa umeme na usambazaji na huduma zingine za matumizi na huduma nyingine ambazo kampuni inatoa.
Rikin Shah, Mkurugenzi Mtendaji wa JCG, akizungumza wakati wa hafla hiyo, alibainisha kuwa:
“JCG Oil & Gas tumefvutiwa na jitihada za TAQA Arabia na Serikali ya Tanzania kutumia rasilimali za taifa za gesi asilia kwa kuanzisha kituo chetu cha kwanza cha TAQA Dalbit. Kupitia ushirikiano wa mradi huu tunaamini kuwa dhamira yetu ya kujenga mustakabali endelevu itatimia.
Utoaji wa mchanganyiko wa gesi asilia na nishati iliyopo itatusaidia kusonga mbele zaidi kwa dira yetu. Tumekuwepo Tanzania kwa miaka 15 sasa tukitoa ufumbuzi wa mafuta kupitia kampuni yetu ya Dalbit Tanzania, iliyoanzishwa mwaka 2008.
Gesi asilia ni chanzo cha nishati safi mbadala ikilinganishwa na petroli na dizeli. Ikija wakati ambapo nchi inakabiliwa na kupanda kwa bei ya mafuta na gharama za maisha, bila shaka wamiliki wa vyombo vya moto watafurahi kujua kwamba kituo hiki cha gesi asilia kitatoa mbadala nafuu na kwamba wanaweza kubadilisha mfumo wa magari yao kwa urahisi katika kituo chetu.