Bobi Wine Asema Maisha Yake Yako Hatarini, Avaa Koti la Kuzuia Risasi Katika Kampeni

Mgombea Urais wa Uganda, kupitia Chama pinzani cha National Unity Platform (NUP), Robert Kyagulanyi Ssentamu, maarufu kama Bobi Wine, amesema maisha yake yako hatarini, hatua iliyomlazimu kuvaa koti la kuzuia risasi wakati wa kampeni zake.
Katika Kampeni zake za hivi karibuni, Bobi Wine na timu yake wamejikuta wakikabiliana na vikosi vya usalama, ambapo kumekuwa na matumizi ya risasi, mabomu ya machozi na kukamatwa kwa baadhi ya wafuasi wake.
Bobi Wine anavituhumu vyombo vya usalama kwa kuingilia mikutano yake, kuziba barabara na kuwakamata wafuasi wake bila sababu za msingi.
Akizungumza kuhusu uamuzi wake wa kuvaa koti la kuzuia risasi, Bobi Wine amesema “Unajua hatari tunayokabiliana nayo kutoka kwa vyombo vya usalama. Tumepokea taarifa kuwa ninaweza kulengwa. Ingawa koti hili halinipi usalama kamili, tunajaribu kupunguza hatari kadri tuwezavyo. Kwa jumla tunajua kuwa Mungu ndiye mwenye nguvu zaidi.”
Hata hivyo Mkuu wa Polisi nchini humo, Abas Byakagaba, amesema kuwa Bobi Wine na wafuasi wake hawafuati miongozo ya Kampeni.
”Tuna wajibu wa kuhakikisha utulivu wa Umma, jambo ambalo ni muhimu kwa uchaguzi wa amani. Hatutakubali vitendo vya uchochezi, matamshi ya chuki, maandamano haramu na kuwashambulia Maafisa wa Usalama.” ameeleza Mkuu huyo.
Kwa upande mwingine, maandalizi ya uchaguzi yanayoendelea Nchini Ugandq unaotarajiwa kufanyika Januari 15, 2026, yanaongozwa na Tume ya Uchaguzi, ambayo imeeleza kuwa inahitaji haraka Shilingi Bilioni 469.5 za Uganda kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kielektroniki vya utambuzi wa wapiga kura.
Stori: Elvan Stambuli, GPL

