The House of Favourite Newspapers

Bongo Muvi, Hii ‘Ngoma Ya Kimasai’ Hadi Lini?

0
Ramsey na Danieline.

NIANZE kwa kuwapa heshima kubwa wacheza filamu wote Bongo, kwa sababu kazi waliyoifanya kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita ni yenye kutukuka na isiyo na shaka ya kupongezwa.

Imetengeneza fani inayoheshimika, inayoajiri na inayokua, ambayo kama mambo yataenda vizuri, yakiongozwa na wanatasnia wenyewe, miaka michache ijayo itaanza kututengenezea mamilionea, kama kule Bongo Fleva ambako sasa wameanza kula matunda ya juhudi zao.

Wanafanya vizuri kwa kweli, kwa sababu pale kabla hawajakaa vizuri, tulipata burudani kutoka kwa waigizaji wa Nigeria, lakini kidogokidogo tukawa tunawaona vijana wetu nao wanafanya vizuri kiasi kwamba miaka ya hivi karibuni waliwasogelea kwa kiwango kikubwa waigizaji hao wa Afrika Magharibi.

Ilifurahisha sana baadhi ya mastaa wao walipoanza kuonekana katika muvi za waigizaji wetu, kama vile alivyofanya marehemu Steven Kanumba ‘The Great’ na Wema Sepetu, maana walituletea watu kama akina Ramsey Nouh, Omotola Jalade na wenzao wa aina hiyo.

Omotola.

Lakini katika hali ya kusikitisha, kwa uzoefu wa fani hii, ukiwatazama sana hawa Bongo Muvi, unawaona kama watu wanaorudi nyuma badala ya kusonga mbele, ingawa kuna waigizaji wengi wanaoendelea kufanya vizuri katika kazi zao, hata kama zitakuwa zimekosa viwango vya ubora unaotakiwa.

Nimezungumza na baadhi ya waigizaji na hata kufuatilia ‘interviews’ za wengine. Kuna kitu kimoja kinazungumzwa nao, ambacho kwao wanakisema kana kwamba hakina madhara, lakini tafsiri inaonyesha kuwa na mwangwi wa kuashiria kurudi kwao nyuma.

Ukiwauliza waigizaji wengi kuhusu nini tatizo katika tasnia yao, watakuambia ni ubinafsi, kutopendana, majungu na vitu vingine vyenye mtazamo hasi. Hakuna anayependa maendeleo ya mwingine, kila mmoja anatanguliza nafsi yake kwanza, ndipo wengine wafuate.

Kwamba waigizaji wote kupendana yaweza kuwa jambo gumu kwa sababu hulka ya binadamu siku zote inatanguliza nafsi, kwa hiyo inaweza isiwe shida sana, lakini umoja na mshikamano ni jambo la kushangaza kwamba halipo.

Kila mmoja kwa wakati wake, anawalalamikia wasambazaji kwamba wanawanyonya na kuwadhulumu, lakini ukirudi nyuma, baadhi yao wanarudisha maneno kwa watu haohao. Tena wanashiriki hata katika kampeni zao.

Wakati waigizaji wengine wakiwalalamikia wasambazaji wa namna hiyo, kuna ambao huwaambii kitu kuhusu hao jamaa, wakiwasifu kuwa bila wao kazi zao haziwezi kupenya mitaani.

Marehemu Kanumba.

Ukiwasikiliza waigizaji wengi, ni kama hawana ‘future’ na kazi hii ya filamu, kwa sababu hawaonyeshi kukataa hali ilivyo sokoni, iwe kwa wasambazaji au kwa walaji wao. Kila kazi mpya inapotoka, inakuja na makosa yaleyale ya sinema iliyotangulia na bahati mbaya zaidi, wanawatumia watu walewale wanaowadhulumu, kwa makubaliano yaleyale ya miaka yote.

Kama wangekuwa watu wenye kuamini kuwa filamu ndiyo kazi za maisha yao, bila shaka wangeweza kubadilika ili kulazimisha mambo yaende sawa. Matokeo yake, hivi sasa kila anayetoa filamu, anatumia mbinu zake kuiingiza sokoni badala ya kutengeneza mfumo ambao ndiyo ungeuza kazi zao.

Waigizaji wengi wanaamini katika kuuza sura, kwamba akishaonekana kwenye filamu na kulipwa kwa kucheza sehemu aliyocheza, inatosha. Ndiyo maana maisha yao halisi nayo yamejaa maigizo.

Wacheza filamu wengi bongo wana biashara za kuchekesha, kama maduka ya nguo, saluni na vipodozi. Hapo ndipo walipoishia, hawaamini kama kwenye filamu, kama wangeijua thamani yake, wao wangekuwa watengenezaji wa nguo na vipodozi wanavyouza.

Wanaiona filamu kama fani ya ziada badala ya kuifanya kuwa namba moja. Marekani na Ulaya, waigizaji wa filamu ni miongoni mwa mamilionea, wanamiliki hisa katika makampuni makubwa.

Kiukweli, wanahitaji mabadiliko makubwa, hasa katika kujitambua na jinsi utajiri ulivyo wazi mbele yao. Wanachohitaji ni umoja na mshikamano kwa sababu fani yao inahitaji timu (team work) laa sivyo wataendelea kucheza ngoma ya kimasai.

OJUKU ABRAHAM | IJUMAA | Za Chembe Lazima Ukae

Leave A Reply