The House of Favourite Newspapers

Boxer Aongezewa Mshahara Yanga

Paul Godfrey ‘Boxer’

NEEMA inazidi kumdondokea beki wa pembeni kinda wa Yanga, Paul Godfrey ‘Boxer’ ambaye mwezi huu anatarajiwa kuongezewa mshahara mpya ndani ya timu hiyo.

 

Hiyo, ikiwa ni siku chache tangu beki huyo achaguliwe kwenye kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars kinachoshiriki Chan ambacho jana kilicheza mchezo wake wa awali na Kenya ‘Harambe Stars’ kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Beki huyo ni mara yake ya kwanza kuitwa kwenye kikosi cha Stars ambaye alipandishwa katika timu ya wakubwa na Kocha Mkuu wa timu hiyo Mwinyi Zahera baada ya kumuamini akitokea U20 ya Yanga.

 

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumatatu, beki huyo mwezi huu ataanza kupokea mshahara wa Sh milioni 1.5. Mtoa taarifa huyo alisema, uongozi umefikia hatua hiyo ya kumuongezea kiasi hicho cha fedha baada ya kuridhishwa na kiwango chake ambacho amekionyesha huku akicheza michezo mingi ya ligi zaidi ya beki mkongwe Juma Abdul.

 

Aliongeza kuwa, beki huyo awali alikuwa akilipwa shilingi 400,000 kwa mwezi ambazo ni ndogo ukilinganisha na kiwango chake. “Ilikuwa lazima Boxer aongezewe mshahara kwani tayari thamani yake imekua katika timu na hiyo ni kutokana na mchango mkubwa anaoutoa.

 

“Hivyo, katika kutambua thamani yake uongozi umemuongezea mshahara kutoka 400,000 kwa mwezi hadi shilingi milioni 1.5 ambazo tumeona zimekidhi viwango vyake,” alisema mtoa taarifa huyo. Alipotafuwa Boxer kuzungumzia hilo simu yake iliita bila kupokelewa kutokana na kuwepo kwenye maandalizi ya mchezo wa Afcon dhidi ya Kenya wa kufuzu Chan.

Comments are closed.