The House of Favourite Newspapers

CHAKULA CHA WAGONJWA NI HIKI

0

CHAKULA CHA WAGONJWA

Nutrient Drinks ni chakula cha wagonjwa kilichobora zaidi

Bila shaka umeshawahi kuugua  ugonjwa wowote kama malaria na aina nyingine. Ukiachilia mbali wengi tuliowahi kuugua muda mrefu na pengine hata kulazwa hospitali kwa maradhi ya aina tofauti katika maisha yetu.

 

Maisha ni safari yenye changamoto nyingi ikiwemo kuugua. Lakini je, unakumbuka jinsi ulivyokosa hamu na nguvu ya kula chochote ulicholetewa na mtu aliyekuuguza? Hali ya kukosa hamu ya kula humtokea kila mgonjwa kwa kuwa, kukosa hamu ya kula ni sehemu ya ugonjwa wowote anaougua binadamu.

 

Hali hiyo hupelekea watu wenye jukumu la kuuguza wagonjwa mahospitalini na hata majumbani, kupatwa na changamoto kubwa kuhakikisha mgonjwa amepata chakula cha kutosha. kwa kuwa mgonjwa asipopata chakula hali yake hudhoofu siku baada ya siku na hatimaye hupoteza maisha.

 

Si kwa ukubwa wa ugonjwa anaougua, la hasha! Bali ni kutokana na mwili kushindwa kupambana na maradhi yake kutokana na njaa. Kwa Tanzania, hili ni tatizo kubwa na wengi hupoteza maisha kwa kuwa wengi wetu tunawauguza wagonjwa bila kujua kitaalamu mgonjwa anahitaji lishe ya aina gani ili aweze kumudu matumizi ya dawa anazopewa na madaktari ambazo nyingi huwa kali, humchosha mgonjwa, na kugeuka sumu kwa kuwa huchochea kudhoofisha afya ya mgonjwa ambaye hapati lishe ya kutosha. hii yote inasababishwa na kutokujua chakula cha wagonjwa kilicho sahihi.

 

Kitaalamu, kama unauguza mgonjwa na hana hamu ya kula chakula, basi unatakiwa umnunulie chakula maalum cha wagonjwa ambacho mgonjwa atakunywa glasi moja tu kwa siku na hakika atafanana kiafya na mtu yeyote aliyekula milo yote mitatu kwa siku.

 

Ukiingia katika maduka ya madawa au maduka makubwa ya vyakula yaani ‘Supermarkets’, utakuta aina nyingi tofauti za vyakula hivi ambavyo ni aina ya maziwa ya unga yaliyoshindiliwa virutubisho takribani vyote tunavyovipata katika vyakula vya kawaida kiasi kwamba, mgonjwa akikorogewa glasi moja tu na akanywa inamfanya awe katika hali njema, na ataweza kutumia dawa bila wasiwasi pia atapona haraka zaidi kuliko yule ambaye hapati chakula cha aina hii ambacho kitaalamu huitwa ‘Nutritional Supplement Drink’ ambacho utakipata kikiwa na majina mbalimbali ya kibiashara madukani.

CHAKULA CHA WAGONJWA

Kutokana na wengi kutojua namna chakula hiki kinavyofanya kazi mwilini, wanakiita ‘dawa’. Ni baada ya  mgonjwa aliyelala kwa kukosa nguvu ya kuamka kwa muda mrefu, alipotumia chakula hiki kwa siku 5 hadi 10, alinyanyuka na kuweza kuongea, na hata kwenda msalani yeye mwenyewe.

 

Hii huonekana kama maajabu, lakini ndiyo teknolojia mpya duniani kote. Ni sababu kuu kwamba watu hukimbilia kutibiwa nchi zilizoendelea kwa kuwa huhakikishiwa kupona haraka kutokana na wataalamu wa lishe (Nutritionist) walioko huko kuwa wengi, wameajiriwa katika mahospitali na hushiriki kikamilifu katika kuhakikisha afya za wagonjwa hazitetereki wanapotumia madawa makali kama vile ‘Antibiotics’ na hata tiba za saratani kama vile ‘Chemotherapy’, ambazo hudhoofisha sana afya za wagonjwa.

 

Chakula cha wagonjwa  kimetengenezwaje?

Chakula hiki ni mkandamizo wa virutubisho (macronutrients) ambazo ni protini, wanga, sukari na mafuta. kimetengenezwa maalum kuwa mbadala wa chakula cha kawaida na sio lazima uumwe ndio utumie kwa kuwa huongeza nguvu za mwili kwa kuujaza mwili virutubisho, madini, vitamin na tindikali muhimu kama vile: ‘amino acids’ ambazo humfanya binadamu aondokewe na sonona ambazo kila mgonjwa huwa nazo anapougua.

 

Lakini pia chakula hiki kimetengenezwa mahususi kwa ajili ya kumpa mgonjwa uzito, nguvu, halafu kina pre-na pro-biotics ambazo husaidia mwili kufanya kazi zake sawasawa ikiwemo umeng’enyaji wa chakula unaoweza kumfanya mgonjwa apate choo sawasawa ili atoe sumu za mwili ambazo zingeweza kumfanya asipone.

 

Kukosa choo ni tatizo kubwa kwa wagonjwa wengi hasa waliopooza, wenye saratani na maradhi mengine yanayowalaza wagonjwa vitandani kwa muda mrefu. Chakula hiki kinaweza kukufanya uwe na afya njema na ujisikie vizuri kila siku kwa kuwa sio rahisi katika maisha ya leo kupata mlo kamili wenye vitamin, madini na virutubisho ambavyo mwili unahitaji ili kukupa afya njema. Chakula hiki kitaweza kuupatia mwili kila hitaji kwa kuwa mchanganyiko wake hujumuisha kiasi kikubwa cha nishati, protini, Omega-3 fatty acids, lakini pia kina viwango vikubwa vya vitamin A, vitamin B1, Vitamin B2 vitamin B3, na vitamin B6 huku kikiwa na vizalishi vya Vitamin D na virutubisho vingine kama ‘Inun’ ambayo ni Pre & Pro-Biotics.

 

Chakula hiki kimetengenezwa kitaalamu ili  kumfanya  mgonjwa apate nafuu, na hapo ndipo huitwa dawa.

 

Kitu cha ziada kuhusu chakula cha wagonjwa

Unapokuwa na mgonjwa ambaye tayari ametumia chakula hiki na akaanza kupata nguvu na hamu ya kula, ni vema ukaanza kumuuliza chakula anachokipenda, kisha mpe kama anavyohitaji ili ale na kiweze kufidia upotevu wa afya yake kwa haraka zaidi, wakati akiendelea kutumia chakula hiki glasi moja kila siku.

CHAKULA CHA WAGONJWA

 

Ieleweke kuwa, mdomo wa binadamu hutamani aina ya chakula ambacho kina virutubisho vinavyohitajika mwilini. Kwa mujibu wa madaktari wa lishe duniani kote, chakula ni aina ya dawa ziitwazo ‘Over the counter medicines’. Hizi ni dawa ambazo binadamu huandikiwa na akili yake badala ya daktari ambaye kwa kawaida humuandikia mgonjwa dawa ziitwazo ‘Conventional Medicines’. Dawa hizi hazitakiwi kutumiwa hovyo. Hivyo, ni muhimu kumsikiliza mgonjwa anapenda kula nini na apewe kwa kuwa kuna dawa ambazo mwili wake unazihitaji kupitia vyakula hivyo.

 

Matumizi  ya chakula hiki cha wagonjwa

Matumizi ya chakula hiki hutofautiana kati ya bidhaa moja na nyingine kwa kuwa, kila kampuni hutengeneza kwa mchanganyiko tofauti. Zipo aina ambazo unashauriwa kutumia vijiko viwili, vitatu, vinne, na kuendelea hadi vijiko sita. Ila kampuni karibu zote huweka kijiko maalum ndani ya mkebe wa chakula hicho kama kipimo maalum na unashauriwa kujaza na kufuta inayozidi juu ili kupata kipimo sahihi.

 

Unga huo unaweza kuuchanganya na maji baridi, ya uvuguvugu, au unaweza ukachanganya na juice au hata maziwa kama utayapata ambayo ni bora zaidi.

 

Ukishakoroga unampa mgonjwa ambaye atakunywa glasi moja kwa siku. Hivyo kama hawezi kula kabisa, unatakiwa uwe unampa kijiko kimoja-kimoja taratibu ili asitapike na baada ya siku 5 ataweza kunywa glasi hiyo kwa muda mfupi zaidi.

 

Akifika siku 10, atapata nafuu, ikiambatana na kushika glasi na kunywa mwenyewe. Chakula cha wagonjwa, kina msaada mkubwa.

 

Angalizo ni kuwa, kila mtu anaweza akatumia chakula hiki isipokuwa wenye mzio wa soya au maziwa kwa sababu chakula hiki kimetengenezwa kwa bidhaa hizi kwa kiwango kikubwa, hivyo wanaweza wakapatwa na matatizo ya mzio kama vile: mwili kuwasha, mdomo kuwaka moto, kichefuchefu na kutapika, kukumbwa na mafua ghafla, kizunguzungu au hata kubanwa na kifua kama maumivu ya ugonjwa wa pumu. Endapo utaona dalili hizo, sitisha matumizi ya chakula hiki na haraka nenda ukamuone daktari ambaye atakupa msaada.

 

Dr. John P. Haule – Dietician

+255 768 215 956

Facebook/john.haule4

 

Leave A Reply